Njiwa akiwa na ujumbe wa barua kama inavyo onekana
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Reli, kati ya Tanzania na Zambia(TAZARA) jana walijikuta katika wakati mgumu na baadhi yao kulazimika kuzikimbia ofisi zao, baada ya ndege aina ya njiwa kukutuwa katika moja ya choo cha ofisi hiyo akiwa amefungwa hirizi shingoni, huku akiwa na barua yenye ujumbe wa onyo kali.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea mapema saa mbili asubuhi katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo eneo la Iyunga Mkoani hapa, hali ambayo mbali na baadhi ya wafanyakazi wake kuzikimbia ofisi, ilisababisha kuibuka kwa mjadala mkubwa dhidi ya tukio hilo.
Mtandao huu ulifanikiwa kushudia njiwa huyo mweusi akiwa nyuma ya choo cha kiume katika eneo hilo la ofisi ya mwajiri, huku akiwa amefungwa hirizi shingoni iliyozungushiwa shanga mchanganyiko wa rangi tatu, ambazo ni Nyekundu, Njano na Nyeupe.
Mbali ya kuwa na hirizi hiyo, pia njiwa huyo alikuwa amebeba barua inayodaiwa kuwa ni ya mmoja wa wafanyakazi wa Mamlaka hiyo (jina limehifadhiwa kwa sababu maalumu) ambaye anadaiwa hivi karibuni kufukuzwa kazi kwa makosa ya ubadhirifu.
Barua hiyo ilikuwa na maandishi mekundu yenye ujumbe ulioandikwa kwa lugha mbili za Kiswahili na kiarabu, ambapo katika maandishi ya Kiswahili yalisomeka :
"Naomba majibu haraka kama mtarudisha binti huyu kazini”. ilisema sehemu ya ujumbe huo, huku ikiwa na orodha ya majina matatu ya viongozi wa shirika hilo.
Mbali na ujumbe huo ukiwa umeandikwa kwa maandishi ya mkono yaliyokolezwa kwa wino mwekundu upande wa nyuma, lakini upande wa mbele kulikuwa na maandishi yakiwa ni barua ya kutaarifiwa kufukuzwa kazi kwa mfanyakazi huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Mwajiri wa mamlaka hiyo kanda ya Mbeya, aliyejitambulisha kwa jina la Mchaba Mgweno, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba waliobaini ni wahudumu wa usafi.
Aliongeza kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo aliwaarifu na wafanyakazi wenzake ambao walikusanyika na kumshuhudia Njiwa huyo mweusi akiwa amedhoofika huku akiwa na barua hiyo yenye vitisho.
Alisema baada ya kushuhudia hali hiyo waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi kilichopo ndani ya shirika hilo, ambapo waliichukua barua hiyo na baadhi ya wafanyakazi hao wakienda kutoa maelezo kituoni hapo.
“Kwa kweli hali hii si ya kawaida, ila kwa sasa siwezizungumzia chochote kwa kuwa hata mimi tukio hili limeniweka katika wakati mgumu na nimeshindwa kuendelea na majukumu yangu ” alisema Mgweno.
Hata hivyo kuliibuka malumbano makali kati ya wafanyakazi wa shirika hilo walioshuhudia tukio hilo, ambapo baadhi yao wakidai kuwa tukio hilo ni la kutengenezwa kwa lengo la kuchafuana.
“Hebu angalia hiyo barua yenyewe mbona ni kivuli (Photocopy), kama ingekuwa ni ya ….wanamtaja mfanyakazi aliyefukuzwa jina limehifadhiwa ingekuwa ni nakala halisi….haiwezekani mambo haya ni kutaka kuchafuana tu” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Lakini baadhi yao waliamini kweli kuwa barua hiyo ilitumwa ili itoe vitisho kwa viongozi wa shirika hilo.
Baadhi ya askari polisi wa kituo cha Tazara walikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wake.
“Ndugu zangu nyie mnajua taratibu za utoaji wa taarifa kwa jeshi hili, maana wapo wahusika, lakini kwa kifupi sisi tulipokea taarifa na tunaendelea kuzifanyia kazi” alisema mmoja wa askari hao.
Hata hivyo, hadi tunapoondoka eneo la tukio majira ya saa sita mchana Njiwa huyo alikuwa bado yupo eneo la tukio.
Njiwa akiwa amedhoofu kwa Baridi akiwa katika choo cha wanaume
Hii ni sehemu alipokutwa Njiwa huyo
Majengo nje ya Ofisi ya Afisa Mwajiri
Baadhi ya wafanyakazi wakielekea eneo la tukio
Afisa Mwajiri (Mwenye shati ya bluu) Na baadhi ya wafanyakazi wakishuhudia tukio
Mashuhuda wakitoka eneo la tukio
Barua iliyoletwa na Njiwa maeneo ya Ofisi ya Mwajiri upande wa mbele na nyuma
Jengo la Ofisi ya Afisa Mwajiri
Stesheni ya TAZARA kituo cha Mbeya
--------------
No comments:
Post a Comment