Thursday, July 18, 2013

MZEE MANDELA ASHEREHEKEA MIAKA 95 LEO HUKU AKIWA MAHUTUTI HOSPITALINI



Afrika Kusini leo wanasherehekea miaka 95 ya kuzaliwa kwa Mzee Nelson Mandela huku rais huyo wa zamani bado yuko mahututi hospitalini.
Ilikuwa ikitabiriwa kwamba shujaa huyo wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi kwamba angeruhusiwa kwenda kusherehekea siku yake ya kuzaliwa lakini bado yuko hospitali kutokana na kurejea maambukizi kwenye mapafu.

Kituo cha Kumbukumbu ya Nelson Mandela na makundi mengine yamewataka watu kujitolea kwa dakika 67 kwa kazi za hisani kukumbukia miaka 67 ambayo Mandela aliitumikia jamii yake.

Umoja wa Mataifa pia umetambua mapambano ya Mandela dhidi ya ubaguzi wa rangi na kusema siku yake ya kuzaliwa ni fursa ya kuenzi urithi wake, na shughuli mbalimbali zimeandaliwa duniani kote.

Siku ya kuzaliwa Mandela, Julai 18, ilitangazwa rasmi kuwa Siku ya Kimataifa ya Mandela na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2009 kama kutambua mchango wake kwa utamaduni wa amani na uhuru.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alisema Siku ya kuzaliwa Mandela mwaka huu imekuja katika wakati wa 'kuakisi kwa kina maisha yake na kazi ya Madiba, huku kiongozi huyo wa aina yake akiwa bado yuko hospitalini'
Aliongeza: "Nelson Mandela alijitolea miaka 67 ya maisha yake kupigania haki za binadamu na haki kwa wote."

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ataadhimisha siku ya kuzaliwa Mandela kwa kutoa michango ya nyumba kwa familia masikini katika eneo la Pretoria.

Mandela alilazwa hospitali mjini Pretoria Juni 8 kwa matatizo ya maambukizi kwenye mapafu yake.

Mapema wiki hii, Rais mstaafu Thabo Mbeki alibashiri kwamba Mandela anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali mapema na kwenda kupatia nafuu nyumbani.

Marafiki ambao walimtembelea wamesema yuko kwenye mashine ya kusaidia maisha kwa ajili ya kusaidia tu kupumua kwa urahisi.

Taarifa rasmi za hivi karibuni kabisa kuhusiana na afya yake zilisema Mandela alikuwa kwenye hali mbaya lakini inayoimarika.

Lakini wote, mke wa Mandela, Graca Machel, na Rais Jacob Zuma wamesema hivi karibuni kwamba Mandela anaendelea vema na matibabu.

Shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi alitumikia miaka 27 gerezani kabla ya kuja kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mwaka 1994.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...