Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo yaNje na Ushirikiano wa Kimataifa, Edward Lowassa, amemtahadhalisha kujiepusha na kauli za kuunga mkono ushoga.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, ameliambia NIPASHE Jumapili ofisini kwake jijini hapa jana kuwa ushoga na hai za ndoa kwa watu wa jinsia moja vinaweza `kuiharibu’ ziara yake hapa nchini.
Mapema wiki hii, Rais Obama alikaririwa akizungumzia masuala hayo yanayotajwa kuwa ni moja ya haki za msingi za binadamu, alipokuwa Senegal, lakini akapingwa.
“Watanzania hawatalikubali na wataendelea kushikilia uhuru na heshima walizojengewa tangu awali, kwamba ushoga na ndoa za jinsia moja havikubaliki,” alisema.
Akiwa Senegal, Rais Obama alitaka serikali za Afrika kutoa haki kwa mashoga kama inavyotoa kwa raia wengine.
“Ninachotegemea, I pray and hope (ninasali na kutegemea) kwamba kuhusu mashoga na ndoa za jinsia moja, Rais Obama hatarudia kauli aliyoitoa kule Senegal,” alisema.
Aliongeza, “ninasema hivi kwa sababu Tanzania hatuamini katika ushoga, na endapo utawalazimisha Watanzania, watakukatalia na kushikilia uhuru na heshima waliyojengewa toka awali.”
AHIMIZA MAPOKEZI MAZURI
Hata hivyo, Lowassa aliwataka Watanzania kuiheshimu na kuitumiavema fursa ya kutembelewa na Rais Obama, hivyo wajitokeze kumlaki kwa wingi.
“Tutambue mataifa makubwa yanakimbilia maslahi ya karne inayofuata, kwa mfano Rais wa China, Xi Jiping siku moja baada ya kuapishwa kwake alikuja hapa nchini, ” alisema.
Hivyo, alitoa wito kwa Watanzania kuhakikisha maslahi na fursa za kiuchumi zinakuwa za kwanza kulindwa, kwa kuwa ziara hiyo itafungua milango zaidi kwa wawekezaji kuja nchini.
Pia, Lowassa alisema ziara ya Rais Obama ni kielelezo cha amani na usalama uliopo, na kwamba itasaidia kuwavutia watalii na wadau wa sekta nyingine za maendeleo kuitembelea Tanzania.
KITUO CHA KIJESHI
Kuhusu hofu na tetesi kuwa ziara hiyo imelenga taifa hilo kuja hapa nchini kufungua kituo cha kujiimarisha kiulinzi, Lowassa alisema Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa tayari nchi hiyo ina kituo cha kijeshi nchini Kenya.
“Tuangalie maslahi yetu tuachane na mitazamo hasi, kama ni kituo cha kijeshi tayari kipo Kenya, tujiulize kwa nini marais wa Marekani Bill Clinton na George Bush walivyofanyaziara zao hapa nchini hawakwenda Kenya,” alisema.
WALINZI WA NDANI KUWEKWA KANDO
Kuhusu ziara hiyo kutumia ulinzi wa kimataifa huku majeshi ya Tanzania yakiwekwa kando kwa ushiriki wa moja kwa moja, Lowassa alisema Rais wa Marekani ana kiwango cha juu cha ulinzi unaosimamiwa na nchiyake pekee.
“Ni sahihi walinzi wetu kukaa pembeni, huyu ni kama Rais wa dunia, lakini hata majeshi yetu yanafanya kazi ya ulinzi lakini sio kwamba yatakaa nyuma tu,” alisema.
SUMAYE: TUMKARIBISHE
Naye, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alisema ziara ya Rais Obama haina ujumbe zaidi ya kuhimiza watu wajitokeze kumpokea.
Hata hivyo, Sumaye alikwepa kuzungumzia kwa undani hatua ya kuwafukuza wafanyabiashara kutoka kandoni mwa barabara, ili kupisha mapokezi ya Rais Obama.
“Ninachokielewa ni kuwa barabara ambazo wanapita viongozi kama Rais Obama zinatakiwa kuwa katikahali ya usalama na hivyo kutakiwa kuboreshwa,” alisema.
LIPUMBA: MAFANIKIO NI MADOGO KIUCHUMI
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, alisema mafanikio ya ziaraya Rais Obama yapo katika kujitangaza kimataifa kuliko kiuchumi.
Profesa Lipumba ambaye ni mchumi aliyebobea, alisema changamoto iliyopo ni kwamba bado biashara kati ya nchi mbili hizo siyo kubwa kama ilivyo kwa nchi kama China na Tanzania.
Alitolea mfano, mwaka 2012 bidhaa za hapa nchini zilizouzwa Marekani zilikuwa na thamani ya Dola milioni 66 ikilinganishwa na zile zilizouzwa China ambapo zilikuwa ni zaidi ya Dola milioni 500.
Alisema bidhaa zilizoagizwa kutoka Marekani zilikuwa na thamani ya Dola milioni 230 huku za kutoka China zikiwa na thamani ya zaidi ya Dola milioni 1,100.
“Utakubaliana nami kuwa mahusiano yetu na China ni makubwa kuliko Marekani licha ya nchi hii kutoa fursa kwetu ambazo hatujazitumia ipasavyo,” alisema
Profesa Lipumba alisema Marekani kupitia mpango wake wa kusaidia Maendeleo ya Afrika (AGOA), ulitoa fursa kwa bidhaa za Afrika kuuzwa nchini humo bila ushuru, lakini Tanzania haikuitumia.
Pia alisema utawala wa George Bush, uliisaidia Tanzania kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Compact (MCC) kupewa Dola milioni 700 kwa ajili ya kusaidia miundombinu na ujenzi wa nyaya za umeme kutoka bandarini hadi Zanzibar.
“Pana uwezekano wa mpango wa pili wa MCC, Tanzania ikapata msaada wa kuimarisha miundombinu ya umeme, lakini pia kampuni za Marekani kuja kuwekeza hapa kwetu,” alisema.
Alisema uwekezaji wa kampuni hizoutategemeana na wafanyabiashara wa hapa nchini pamoja na serikali kutumia fursa mbalimbali za nchi hiyo.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema ili nchi iweze kujikwamua na umasikini itatokana na jinsi itakavyotumia sera na juhudina siyo kutegemea msaada kutoka nje.
HOTELI ZIMEJAA
Wingi wa wageni wakiwamo watakaofika kwa ajili ya ziara ya Rais Obama, umesababisha hoteli nyingi za jijini Dar es Salaam `kujaa’.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili ulibaini kwamba kwa zaidi ya wiki sasa, hoteli nyingi hazikupokea wageni kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, nyingine zililipiwa ingawa vyumba havikutumika kwa wakati.
POLISI: WASIO NA KAZI WASIJE MJINI
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, amewataka wananchi ambao hawatakuwa na mambo muhimu ya kufanya katikati ya jiji, wasifike huko kupunguza msongamano wa watu na magari baada ya kuwasili kwa Rais Obama.
Alisema, baadhi ya barabara zitafungwa kwa muda kwa ajili ya viongozi kuzitumia, hivyo kusababisha msongamano.
Hekaheka zimetanda jijini Dar es Salaam, ikiwa ni zaidi ya saa 24 kabla ya kuwasili kwa Rais Barack Obama.
Rais Obama, atawasili nchini kesho akitokea Afrika Kusini, ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumza katika mkutano wa ‘viongozi vijana wa Afrika’ na kujibu maswali kutoka nchi tofauti.
Mkutano huo ulifanyika jana jioni huko Soweto nchini Afrika Kusini, ambapo alipokewaa na kujibu maswali kutoka Kenya, Uganda, Nigeria na Afrika Kusini kwenyewe.
Jijini Dar es Salaam, shughuli kadhaazikiwamo za ulinzi na usalama, zinafanyika kwa kasi na umakini kuhakikisha ziara ya Rais Obama inafanyika pasipo bughudha. kujibu maswali kutoka Kenya, Uganda, Nigeria na Afrika Kusini kwenyewe.
Jijini Dar es Salaam, shughuli kadhaazikiwamo za ulinzi na usalama, zinafanyika kwa kasi na umakini kuhakikisha ziara ya Rais Obama inafanyika pasipo bughudha.
Hata hivyo, sehemu kubwa inayohusu masuala ya itifaki, ulinzi na usalama yanafanywa na taasisi za Marekani, kwa kuzishirikisha taasisi za ndani kwa kiwango kidogo.
“Hawa jamaa (Wamarekani) wanapoingia nchi yeyote wakiwa naRais wao, shughuli nyingi na uamuzi wanafanya wao, sisi wa ndani inakuwa kushirikishwa kwa kiasi kidogo,” kilieleza chanzo cha NIPASHE Jumapili kutoka moja ya taasisi zinahusika katika ziara hiyo.
Maeneo kadhaa ya jijini humo, yaliendelea kudhibitiwa kwa ulinzi mkali na doria za mara kwa mara, huku kandoni mwa baadhi ya barabara wakionekana askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Mathalani, kandoni mwa barabara ya Morogoro, eneo la Ubungo, walionekana askari wa JWTZ maarufu kama MP.
Shughuli nyingine zimehusisha pia operesheni zinazofanywa na polisi kwa kusaidiana na mgambo wa jiji, kuhakikisha watu na bidhaa zilizopokandoni mwa barabara zitakazotumika kwa ziara ya Rais Obama, vinaondolewa.
Magari yaliyowabeba polisi wenye silaha za moto na mabomu ya machozi, yalionekana katika mitaa kadhaa jijini humu, wakihakikisha operesheni hiyo inafanyika pasipo kikwazo kutoka kwa wahusika.
Kila palipofanyika operesheni hiyo, baadhi ya askari walifanya doria zamu kwa zamu, kuhakikisha kuwa bidhaa na watu walioondolewa, hawarejei.
Hata hivyo, waathirika katika operesheni hiyo walieleza kutofurahia, huku wakihoji ni kwa nini serikali haikuwaandalia mazingira mbadala kabla ya utekelezaji wake.
Walisema miongoni mwao, wamekopa mitaji kutoka kwenye taasisi za kifedha, hivyo kusimamisha biashara zao ili kupisha ujio wa Rais Obama, kutawaweka katika hali ngumu kiuchumi.
“Ikiwa ujio wa Rais Obama unatutesa wafanyabiashara kiasi hiki, ni vigumu kuhimili maisha yetu, kwa sababu hatujui hatma yetu baada ya yeye kuondoka,” alisema mfanyabiashara Zena Rashidi wa Kariakoo.
Hata hivyo, wamachinga walionekana jana katika kituo cha mabasi cha Mwenge walipofukuzwa, wakiwa wanaendelea na biashara zao.
Lakini walifanya hivyo kwa tahadhali ikiwamo kushika bidhaa chache mikononi, huku wakitumia ‘janja’ ya kupiga kelele za ‘kumsifia’ Rais Obama.
Walisikika miongoni mwao wakisema, ‘praise to Obama’ na wengine wakaitikia ‘aaamen’. Walifanya hivyo zamu kwa zamu, lakini haikujulisha waliashiria nini.
BARABARA ZAPAMBWA
Aidha, barabara zote atakazopita Obama wakati wa ziara yake zimepambwa kwa bendera za Marekani na Tanzania; huku zikinakshiwa kwa picha yake ambayo imeandikwa ‘President Barack Obama’ karibu Tanzania.
Barabara hizo ni ile ya Nyerere kuanzia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Mwai Kibaki na Bagamoyo.
NIPASHE Jumapili imeshuhudia pichana bendera hizo zikiwa zimewekwa kwenye mabango yote yaliyo barabarani kuanzia Ikulu hadi kwenye barabara hizo huku usafi wa jiji ukionekana kuimarika zaidi.
Jana gazeti hili lilishuhudia karibu barabara zote, vijana wanaofanyakazi ya kuweka bendera na picha ya Obama wakifanyakazi hiyo.
No comments:
Post a Comment