Saturday, July 13, 2013

Kaburi la watu 917 labainika


Humme alisema kuna mpango wa Serikali ya Rwanda kufukua mabaki ya miili hiyo ili ikafanyiwe maziko nchini mwao.

Ngara. Timu ya kwanza kati ya 14 za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyowasili Ngara kuratibu maoni ya Katiba Mpya yanayotolewa na mabaraza ya Katiba ya Wilaya, imepokewa kwa kupelekwa kushudhudia kaburi la pamoja la Wanyarwanda lililopo wilayani hapa.

Akiwakaribisha, Kaimu Mkurugenzi Wilaya ya Ngara, Herman Humme, alisema licha ya kazi iliyowapeleka, aliomba watembelee kaburi hilo lililotokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.

“Baada ya watu kuuawa, miili yao ilitundikwa kwenye miti mithili ya mishikaki... naomba msiondoke bila kushuhudia kaburi walimozikwa watu 917 ambao waliopolewa majini,” alisema Humme.

Humme alisema kuna mpango wa Serikali ya Rwanda kufukua mabaki ya miili hiyo ili ikafanyiwe maziko nchini mwao.

“Licha ya kwamba mmekuja kwa kazi nyingine, nawaomba msiondoke bila kutembelea kaburi hilo,” alisema Humme.

Naye kiongozi wa timu hiyo, Dk Sengodo Mvungi, alipendekeza mpango wa kuhamisha miili hiyo usitekelezwe ili Tanzania nayo ibaki na historia hai ya tukio hilo, kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

“Wanyarwanda wanaweza kuruhusiwa kuboresha mazingira lilipo kaburi hili na kulitumia kama sehemu ya historia ya nchi yao ndani ya Tanzania,” alisema Dk Mvungi na kuongeza:

“Siyo kuhamisha kwa sababu hata Tanzania inahitaji kumbukumbu hai, inayodhihirisha wema wake.”

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume, timu hiyo imeanza kazi zake jana wilayani Ngara na itaratibu kazi za Mabaraza ya Katiba ya Halmashauri 13 ndani ya wilaya 11 za mikoa ya Kanda ya Ziwa; Kagera, Geita na Mwanza.

Wilaya hizo zinatajwa kuwa ni Ngara, Karagwe, Kyerwa, Misenyi, Bukoba, Muleba, Chato, Geita, Nyang’hwale, Sengerema na Biharamulo.

Halmashauri ambazo itaratibu ni Ngara, Karagwe, Kyerwa, Misenyi, Bukoba, Muleba, Chato, Sengerema, Nyang’hwale, Biharamulo, Geita na miji ya Geita na Bukoba.

Mabaraza ya katiba yalianza kazi nchini jana, yatapitia Rasimu ya Katiba na kutoa mapendekezo ambayo yatawasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...