Monday, July 29, 2013

DK SLAA AMWEKA KITIMOTO NCHIMBI-ZUIA UHALIFU SIO UPINZANI


 
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi jana alikuwa na wakati mgumu katika Kongamano la Amani lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa kumtaka ajiuzulu kutokana na kushindwa kudhibiti uhalifu nchini.
Mbali ya Dk Nchimbi, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi katika kongamano hilo, Brigedia Jenerali, Elias Athanas naye alibanwa akitakiwa kueleza tuhuma za askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuhusishwa na vitendo vya ubakaji na utesaji wa raia mjini Mtwara.
Akizungumza katika kongamano hilo, Dk Slaa alisema hakuna haja ya kutafuta mchawi wa amani ya nchi bali, Serikali inapaswa kulaumiwa kutokana na watendaji wake kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Alitoa mfano wa kitendo cha Bandari ya Dar es Salaam kutumiwa kupitisha pembe za ndovu wakati maofisa polisi wakiwemo ni kitendo cha aibu ambacho kinatosha kumfanya Waziri Nchimbi ajiuzulu.
Akijibu madai hayo wakati akihitimisha kongamano hilo, Waziri Nchimbi alikiri kuwa baadhi ya polisi wamekuwa na tabia ya kujihusisha na rushwa na katika kupambana na hali hiyo, Serikali imeshawatimu kazi askari 101 katika kipindi cha mwaka 2012.
Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema suluhisho la matatizo yaliyopo ndani ya Jeshi la Polisi siyo kuwatimua kazi askari pekee na ndiyo maana Serikali imeanza mkakati wa kutoa mafunzo ya maadili ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa weledi.
Alisema ataendelea kupokea changamoto kutoka kwa wadau wote wa amani na kupongeza waliobuni kongamano hilo, huku akiahidi kutoa ushirikiano kufanikisha jambo lolote linalohusiana na mjadala wa amani ya nchi.
Kuhusu ubakaji na utesaji wa wanajeshi, Dk Slaa alisema inasikitisha kuona jeshi ambalo linapaswa kulinda amani linatesa na kuwabaka raia.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro ambaye alisema anao ushahidi wa wanachama wa chama chake waliojeruhiwa na kupakwa pilipili akisema kwamba jeshi hilo limekuwa na baadhi ya askari wakatili tofauti na misingi ya kuanzishwa kwake.
Akijibu tuhuma hizo, Brigedia Jenerali Athanas alikanusha madai hayo akisema siyo kweli kwamba JWTZ linaendesha unyama na kwamba lipo Mtwara kwa ajili ya kulinda amani na kusema tuhuma hizo ni za mitaani.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alidai kuwa tangu nchi ilipopata uhuru haijawahi kuwa na amani ya kweli akitoa mfano wa wananchi kuhamishwa kwa nguvu katika maeneo yao.
Alisema katika siku za karibuni, tofauti na zamani polisi ilipokuwa ikifanya kazi ya kudhibiti uhalifu, sasa inaonekana kama kazi yake ni kudhibiti upinzani na limekuwa likituhumiwa mara kwa mara kwa kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kusababisha mauaji.
Alipiga kijembe akisema kwamba CCM kinakaribia kuanguka na ndiyo maana kimekuwa kikitumia mabavu kudhibiti upinzani.
Awali, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gaudence Mpangala alisema amani inaweza kutoweka ikiwa CCM kitaendelea kutumia dola kudhibiti upinzani.
Alisema CCM kinapaswa kufanya kazi kama ilivyo vyama vingine vya siasa na kuonya kwamba hata kukiwa na makongamano mengi, amani haitapatikana kama hakitajitathmini na kuchukua hatua.
Alisema polisi imekuwa ikifanya makosa kuzuia maandamano ya vyama vya upinzani akisema sheria iko wazi ikisema vinachotakiwa kufanya ni kulitaarifu jeshi hilo kuhusu ratiba ya shughuli zake.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...