Monday, June 24, 2013

Wamiliki wa mabasi Arusha, Kilimanjaro kugoma leo


 
Dk Abdallah Msengi - Mkuu wa Wilaya ya Moshi


Mgomo huo unatarajiwa kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa wananchi.

Dar es Salaam. Chama cha Wamiliki wa Mabasi katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (Akiboa), leo wanaanza mgomo kwa kutobeba abiria kupinga magari ya Noah kuruhusiwa kubeba abiria 14 kinyume na sheria.

Uamuzi wa kuanza kwa mgomo huo ambao unatarajiwa kusababisha tatizo la usafiri katika mikoa hiyo ulifikiwa juzi katika kikao cha wanachama wa Akiboa.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu alisema mgomo huo ni kupinga uvunjaji wa sheria zilizowekwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) zinazotaka magari ya Noah kubeba abiria saba.

“ Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wamewaruhusu wenye magari ya Noah kusafirisha abiria zaidi ya 14 ingawa kisheria gari hizo zinatakiwa kubeba abiria saba, huu ni uvunjaji wa sheria na tunaupinga,” alisema Mrutu.

“Hapa kuna mambo yanafanyika kienyejienyeji, tunachopinga hapa ni kuhalalishwa kwa magari haya kubeba abiria wakati hayana leseni ya kufanya hivyo, kuna magari yamekata leseni zote, yanalipa kodi zote kuanza TRA,halmashauri, Sumatra na nyingine nyingi na zinabanwa, lakini kwa magari haya tunaona wanafanya biashara bila hata kulipa kodi stahiki,” alisema.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alikaririwa akiwaruhusu wenye magari ya Noah kubeba kiasi hicho cha abiria na kwenda umbali wowote ingawa Sumatra inawataka kwenda kilometa zisizozidi 50.

Alisema hata Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kilimanjaro, Dk Abdallah Msengi alitoa ruksa hiyo kwa wenye Noah kufanya biashara ya kuchukua abiria.

“Viongozi wa serikali katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kuungana na wamiliki wa magari ya Noah inatia mashaka, tunaona hapa kuna tatizo kwa viongozi hawa,” alisema.

Alisema Taboa na Akiboa wanasikitishwa na hatua ya viongozi hao wa Serikali kupinga wazi sheria halali ya Sumatra.

Alisema magari ya Noah hayana leseni ya biashara,lakini viongozi hao wanatoa maagizo kuyaruhusu kufanya safari zake sehemu zozote ile bila kujali ya umbali na idadi ya abiria.

“Hata huko zilipotengenezwa Japan mwisho wa kubeba ni watu saba iweje hapa Tanzania, Kuna picha inayojengeka hapa kwani hata katika kikao kilichofanyika Juni 19, mwaka huu mkoani Kilimanjaro wenye magari haya wamekuwa na jeuri kuliko Sumatra,” alisema Mrutu.
Mkoa wa Arusha ni kati ya mikoa inayoongoza kwa kuwa na magari mengi aina ya Noah yanayofanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka na kwenda maeneo mbalimbali ya mji huo wa kitalii.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...