Dar es Salaam. Mbunge wa
Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amemtuhumu Mbunge wa Monduli
Edward Lowassa kwamba anahusika na kipigo alichokipata kutokana na
chuki aliyonayo kwake.
Aidha amemtuhumu Spika wa Bunge, Anne Makinda
kwamba naye ni miongoni mwa watu wanaomchukia pamoja na viongozi wengine
wa Bunge, kwa kuwa hakuna kati yao aliyempigia simu au kumtumia ujumbe
wa kumjulia hali kutokana na kipigo alichopata ambacho kimemsababishia
maumivu makali.
Akizungumza jana akiwa kwenye chumba alicholazwa
katika Taasisi ya Tiba ya Magonjwa ya Mifupa na Ufahamu Muhimbili (Moi),
Nassari alidai Lowassa ambaye amewahi kuwa waziri mkuu kabla ya
kujiuzulu, amemchukia tangu alipomshinda mkwewe Sioi Sumari, kwenye
uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Aprili mwaka jana.
Nassari aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya
Selian ya jijini Arusha kabla ya kuhamishiwa MOI, alidai kupigwa na
kuchaniwa nguo na Green Guard wakati alipokuwa katika jitihada zake za
kuhesabu kura kwenye uchaguzi wa udiwani wa Kata ya Makuyuni-Monduli.
“Kipigo nilichopata Lowassa anahusika ananichukia,
anataka urais lakini hawezi kuupata kwa kuuumiza watu kama hivi,
alifikiri kwamba nitakufa sitakufa hadi kwa mapenzi ya Mungu,” alisema.
Alisema kuna jambo ambalo wananchi wanapaswa
kulifikiria ni jinsi ambavyo kumekuwa na matukio ya kutekwa na kuvamiwa,
lakini hakuna yanayohusisha kiongozi wa CCM, badala yake ni raia wa
kawaida na viongozi wa dini na siasa. Nassari alidai akiwa kama wakala
mkuu wa Chadema katika kata hiyo, alikumbana na mambo kadhaa
yaliyomshangaza, ikiwa ni pamoja na kufanyiwa jaribio la kutekwa mara
mbili, kabla ya kushambuliwa kwa kipigo.
Alisema pia anashukuru kwamba askari wawili
waliokuwepo katika eneo hilo walijitahidi kutaka kumnusuru, lakini
walizidiwa nguvu na vijana hao, hasa kutokana na kutokuwa na bunduki,
ambapo yeye alipofanikiwa kuchoropoka alikimbilia bastola yake na
kuwanyoshea vijana hao bila kufyatua.
Akizungumzia kuhusu hali yake, Nassari alisema
amepimwa kipimo cha X-ray ambapo imeonyesha kuwa pingili za mgongo wake
zipo sawa, lakini daktari ameshauri afanyiwe kipimo kingine kiitwacho
MRI ili kuangalia hali ya mishipa kutokana na maumivu makali
anayoendelea kuyapata.
Aidha alitumia fursa hiyo kumshukuru Mbunge wa
Kuteuliwa, Joseph Mbatia kuwa ndiye aliyemsaidia kufanya mipango
kuwasiliana na uongozi wa Bunge na kumwezesha kuhamishiwa Moi, baada ya
wabunge wote wa Chadema kwenda Arusha kushughulikia waliofariki kwa
bomu.
Hata hivyo, Lowassa alipotafutwa kuhusiana na
tuhuma hizo alikataa kuzungumzia suala hilo na kusema hilo aulizwe
Msimamizi wa Uchaguzi, Paulo Kitaleki.
Mwananchi ilimtafuta Kitaleki ambaye pia ni katibu
tarafa, alikanusha kuhusika kwa Lowassa akielezea kuwa siku ya tukio
hilo alikuwa Geita.
“Huyu Nassari ni mwigizaji na anafaa kuwa msanii
kwa kuwa anaigiza tu hata hakupigwa, bali yeye ndiyo aliyempiga Wakala
wa CCM, Hussein Osama ambaye ni mlemavu, kisha akatimua mbio baada ya
vijana kutaka kumkamata, nashangaa kumwona yupo hospitali akidai
kupigwa, siyo kweli,” alisema Kitaleki.
No comments:
Post a Comment