Friday, March 8, 2013

HANS POPPE AJIUZULU NYADHIFA ZOTE SIMBA SC




Hans Poppe; Ameachia ngazi Simba SC

ZACHARIA Hans Poppe, amejiuzulu wadhifa wa Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC ya dar es Salaam pamoja na Uenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo leo.
Kwa mujibu wa habari ambazo zimetufikia  kutoka ndani ya Simba mida hii, Hans Poppe amewasilisha barua ya kujiuzulu leo akielezea kusitikishwa kwake na hali halisi ndani ya klabu.
Alipoulizwa mwenyewe kuhusu hilo, alisema; “Sipo katika nafasi ya kulizungumzia hilo kwa sasa, wasiliana na Katibu (Evodius Mtawala) au Mwenyekiti (Alhaj Ismail Aden Rage),” alisema Hans Poppe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Friends of Simba na kukata simu.
Mtawala na Rage hawakupatikana kwenye simu zao mida hii, ingawa tunaendelea na juhudi za kuwatafuta.
Kwa mujibu wa barua hiyo, pamoja na kujiuzulu, Hans Poppe ameahidi kuendelea kuwa mwanachama mwaminifu ndani ya Simba SC.
Wazi kujiuzulu kwa Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ni pigo kwa klabu hiyo, kwani alikuwa akiisaidia mno kwa hali na mali.
Aidha, kujiuzulu kwa Hans Poppe wazi kutachochea zaidi mgogoro ndani ya klabu hiyo na kuongeza shinikizo la viongozi wa klabu hiyo kujiuzulu pia.
Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya kwanza tu.
Ubingwa wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 36 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 42, zote za Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...