Thursday, February 21, 2013

HIVI NDO VITUKO AMBAVYO BAADHI WANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE WALIANDIKA KATIKA KARATASI ZA MAJIBU


Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako akionyesha karatasi ya majibu ya mmoja wa watahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2012, Dar es Salaam jana.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaweza kukumbwa na kashfa kubwa kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne ya 2012 yaliyotangazwa juzi na Waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa.


Kashfa hiyo inatokana na aina ya majibu yaliyoandikwa na baadhi ya watahiniwa katika mitihani hiyo, huku wengine wakikusanya vitabu vya majibu bila kujibu chochote, hali inayohusishwa na uhaba mkubwa wa walimu katika baadhi ya shule za sekondari nchini.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako alisema wasahihishaji walikutana na mambo ya ajabu yakiwamo matusi, michoro ya vitu visivyoeleweka, mashairi na nyimbo za muziki wa kizazi kipya (bongo fleva).

“Mwaka jana tulikutana na ‘single’ yaani waliandika mashairi kwa uchache, lakini mwaka huu tumepata albamu nzima… ni vituko vitupu, wengine wanaandika mapenzi, mwanafunzi anatumia ukurasa mzima kumlalamikia mpenzi wake. Miongoni mwa yaliyoandikwa ni mpenzi, umeniacha, natamani kunywa sumu, usiku silali nakuwaza wewe…” alisema Dk Ndalichako.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Ndalichako alisema wanafunzi wengine waliandika malalamiko dhidi ya wabunge na uendeshaji wa Bunge.

“Unakuta mwanafunzi anaeleza anavyolishangaa Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge, wamekaa kama wapo kijiweni, wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za wananchi waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda Kombe la Kagame inapokelewa bungeni.

Bunge limekuwa kama kijiwe, bungeni siyo ukumbi wa starehe kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika ofisi zao au viwanjani…” alisema.

Alisema wanafunzi walioandika vitu visivyoeleweka walikuwa ni wengi na walichangia kwa kiasi kikubwa matokeo kuwa mabaya.
Dk Ndalichako alionyesha baadhi ya michoro hiyo ambayo inaonyesha vikaragosi ambavyo wanafunzi hao waliviita Messi (Lionel, mchezaji wa Barcelona) na zombi (ni picha za kutisha) ambazo huonyeshwa kwenye televisheni.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...