HABARI za tetesi zilizotapakaa katika mitaa ya jijini hii leo ni kutokana na kutokomea kusikojulikana kwa mchezaji wa kimataifa, Mrisho Ngassa, na kutojitokeza kwa ajili ya kufanya taratibu za uhamisho wake wa kimataifa kwenda Sudan, ni kutokana na uamuzi alionao mchezaji huyo wa kuamua kurejea katika Klabu yake ya zamani ya Yanga.
Wakati muda uliotolewa na msemaji wa Klabu ya El Merreikh ya Sudan, ukiwa unazidi kuisha kabla mchezaji huyo kujitokeza na kumaliza taratibu za usajili huo wa kimataifa, imeelezwa kuwa hadi sasa Ngasa bado hajapatikana na kwamba simu zake zote hazipatikani hewani.
Chanzo cha habari hizi kilicho karibu na mchezaji huyo na klabu ya Yanga, kimeeleza kuwa, Ngassa tayari amekubaliana Klabu yake ya zamani ya Yanga na kwamba atajiunga na klabu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo wa miezi sita alioubakisha na klabu ya Simba kwa malipo mazuri kama ambavyo imekuwa kwa mchezaji Haruna Niyonzima.
"Ni kweli Ngassa tayari ameshakuwa na mazungumzo ya awali na Yanga kwa miaka miwili, na tayari hivi sasa ameshapewa Sh. millioni 10 na fedha nyingine atapewa mara atakapomaliza mkataba wake na Simba mwishoni mwa msimu.
Sasa hivi Ngasa amejificha ili kuepeuka usumbufu wa viongozi wa El Merreikh na Simba pamoja na Azam." kilisema chanzo hicho
Mrisho Ngassa amekuwa gumzo kubwa kwenye vyombo vya habari kuhusiana na usajili wake kwa timu ya El Merreikh ambao walimuahidi mshahara wa Dola 4000 kwa mwezi pamoja na Dola 75000 kama ada ya usajili, huku vilabu vyake vya Simba na Azam FC vikilipwa Dola 100,000.
Kutokana na tukio hilo la kupotea kwa Ngasa, huku timu ya El merreikh, ikimsubiri mchezaji huyo ili kujitokeza kwao na kumaliza taratibu za usajili huo, tayari Uongozi wa Klabu hiyo umetoa tamko .
Msemaji huyo wa El Merreikh, Shekhe Idrissa, alesema kuwa tayari Klabu hiyo ilishafanya makubaliano na vilabu vya Azam FC na Simba SC na mchezaji huyo na kilichokuwa kimebaki ni kupatikana kwa mchezaji huyo na kutia saini mikataba pamoja na kufanya vipimo vya afya ili mchezaji huyo aweze kujiunga na timu hiyo tajiri ya Sudan, lakini muda mfupi baada ya kufika Dar es Salaam mchezaji huyo amekuwa mafichoni - akiwa hapokei simu na muda mwingine anazima bila kutoa taarifa zozote kwa vilabu husika.
"Mrisho Ngassa tulikuwa tumeshafanya nae mazungumzo vizuri na tukakubaliana na ikabakia kumalizana na vilabu vya Simba na Azam, lakini sasa tukiwa tayari tumemalizana na vilabu mchezaji mwenyewe amekuwa akifanya vitendo visivyo vya kistaarabu, simu yangu hapokei na muda mwingine anaizima kabisa''. alisema Shekhe
Hili sio jambo zuri kabisa kwake na kwa mpira wa Tanzania kiujumla. Anaharibu sifa ya wachezaji wenzie wa kitanzania, ni vizuri angepokea simu na kutueleza kama dili linawezekana au tofauti, kuliko kutuacha sisi tukipoteza muda kuwepo hapa Tanzania huku tukiwa njiapanda bila kujua kinachoendelea.
Kwa tabia hii ya Ngassa tumefikia maamuzi ya kwamba mpaka kesho asubuhi (LEO) kama hatapatikana, tutasitisha uhamisho wa mchezaji huyu na kuangalia sehemu nyingine mbali na Tanzania." - Alimaliza Shekhe Idrissa.
Taarifa zilizoenea ni kwamba Ngassa hataki kwenda El Merreikh baada ya kushawishiwa na viongozi wa Simba ili aendelee kuwepo Simba mpaka mkopo wake utakapoisha mwakani na aweze kujiunga na klabu hiyo yake ya zamani.
No comments:
Post a Comment