Tuesday, October 9, 2012

NHIF kumuenzi Baba wa Taifa kipekee




KATIKA kuhakikisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anaenziwa kipekee, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaendesha zoezi la upimaji afya za wanachama na wananchi kwa ujumla mkoani Shinyanga ambako kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika Oktoba 14, mwaka huu.

Akizungumzia zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji Eugen Mikongoti alisema kuwa, Mfuko umefikia uamuzi huo kwa lengo la kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na Baba wa Taifa enzi za uhai wake.

“Baba wa Taifa aliapa kupigana na maadui watatu ambao ni Umasikini, Ujinga na Maradhi na katika hayo sisi ni wadau wakubwa katika kupambana na adui maradhi na ndio maana tumeona tumuenzi kwa njia hii ambapo wananchi watapima afya zao bila malipo na kupata ushauri wa kitaalam ili kuepukana na maradhi yasiyoambukiza,” alisema Mikongoti.

Mbali na upimaji wa afya kwa wananchi, alisema kuwa Mfuko unatumia fursa hiyo kujibu kero mbalimbali za wanachama wake ambao watafika katika viwanja vya Sabasaba ambako Mfuko umeweka banda kwa ajili ya kuendesha zoezi la upimaji na utoaji wa elimu juu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii, kwa muda wa siku tano, kuanzia jana.

Alisema kuwa lengo kubwa la NHIF ni kuhakikisha wanachama wake na wananchi kwa ujumla wanapata huduma bora za matibabu na Vituo vya kutolea huduma hizo vinaboreshwa kwa kuwa na vifaa vya kisasa vya uchunguzi kupitia fursa inayotolewa na Mfuko huo ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo.


“Mfuko umekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha huduma za afya vituoni zinakuwa bora na unafanya hivyo kwa kutambua kuwa mhimili mkubwa wa Mtanzania katika kufanya kazi na kujiondolea umasikini ni afya yake kwanza…nawaomba wananchi wa Shinyanga na wa maeneo mengine mfike katika banda letu ambalo linatoa huduma za upimaji na elimu ya afya kwa ujumla,” alisema.

Mikongoti alisema kuwa Mfuko utaendelea kumuenzi Baba wa Taifa katika kupambana na adui maradhi kwa kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa matibabu kupitia utaratibu wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii.


Wakati huo huo, Mfuko umeendelea na jitihada zake za kuhakikisha makundi maalum yanapata huduma bora baada ya kuchangia jumla ya shilingi milioni 1.5, shuka 80 na fulana 80 kwa Kituo cha Mihuji Chesire Home kilichopo mjini Dodoma ambacho kinalea watoto wenye matatizo ya mtindio wa ubongo.

Mchango huo wa NHIF ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma katika harambee ya kuchangia kituo hicho na Meneja wa Kanda ya Kati Dkt. Daudi Bunyinyiga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Emanuel Humba.

Akiwasilisha mchango huo, Dokta Bunyinyiga alisema kuwa Mfuko kama Taasisi inayofanya kazi na Jamii inawajibu wa kuhakikisha jamii inayoizunguka hususani watu wenye mahitaji maalum wanafaidika na huduma zake.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...