Thursday, September 13, 2012

POLISI KIZIMBANI KWA MAUAJI YA MWANGOSI


Mtuhumiwa, Pasificus Cleophace Simon (23), akifyatua bomu linalosadikiwa kumuua aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten Mkoa wa Iringa, Daudi Mwangosi.
NI PC PASIFICUS CLEOPHACE SIMON (23) KIKOSI CHA FFU



HATIMAYE askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, amefikishwa mahakamani kwa shitaka la mauaji.

Askari huyo mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simon (23), mkazi wa FFU Manispaa ya Iringa, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi ya Wilaya jana akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Mwangosi.

Mashtaka hayo alisomewa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Michael Luena.

Luena alidai mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Dyness Lyimo, kuwa Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, mtuhumiwa huyo alimuua Mwangosi, kinyume cha kifungu cha sheria namba 148 (5A) (i) cha makosa ya jinai.

Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji kisheria.

Mtuhumiwa alirudishwa mahabusi kutokana na kesi yake kutokuwa na dhamana kisheria.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 26, mwaka huu, itakapotajwa mahakamani hapo.

POLISI WAZUIA WAANDISHI KUMPIGA PICHA

Askari saba waliompeleka mtuhumiwa huyo mahakamani waliovalia kiraia, waliweka ulinzi mkali na kuhakikisha mtuhumiwa hapigwi picha.

Kutokana na hali hiyo, waandishi wa habari walipata wakati mgumu kumpiga picha mtuhumiwa huyo.

Kila walipojaribu kutaka kufanya hivyo, walijikuta wakisukumwa na askari hao kuzuiwa wasimpige picha mtuhumiwa huyo.

Mtuhumiwa huyo alipelekwa kwa mwendo wa haraka kwenye gari lenye namba za usajili T320 ARC aina ya Toyota Land Cruiser GX tofauti na kawaida ya gari linalotumiwa na mahabusu pindi wanapofikishwa mahakamani.

Kadhalika mtuhumiwa huyo alifunikwa kitambaa sehemu za kichwani na kuvalia koti la rangi nyeusi, kiasi cha kumfanya ashindwa kutembea vema.

Hali hiyo ilisababisha kiatu chake kimoja aina ya sandozi kukatika na kubaki katika eneo la viwanja vya mahakama hiyo baada ya gari lililombeba kuondoka eneo hilo.

Mwangosi aliuawa akiwa kazini baada ya kupigwa na bomu lililosambaratisha sehemu kubwa ya mwili wake.

Alikumbwa na mkasa huo wakati polisi wakiwatawanya viongozi, wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ILI kuwazuia wasifungue tawi la chama hicho katika Kata ya Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.

Mauaji ya mwandishi huyo yalilaaniwa vikali na makundi kadhaa ya jamii, ambao walitaka uchunguzi huru ufanyike kubainisha hasa chanzo cha kadhia hiyo.

Miongoni mwa wadau waliojitokeza kupinga na kulaani kwa nguvu zote mauaji hayo, ni Chadema.

Chadema kilipendekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, IGP Mwema, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Kamishna Paul Chagonja, wawajibike kwa kujiuzulu nafasi zao, kutokana na mauaji ya raia katika mikoa ya Morogoro na Iringa kutokea mikononi mwa jeshi hilo, ambalo lipo chini ya usimamizi wao.

Walisema iwapo viongozi hao watashindwa kuwajibika, basi Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi.

Pia walitaka Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Michael Kamuhanda, pamoja na Mkuu wa FFU mkoani humo, wawajibike kwa kujiuzulu kwa sababu hiyo.

Wakati sauti hizo zikipazwa, waandhishi wa habari karibu nchini kote, juzi na jana walifanya maandamano ya kimya kimya kulaani mauaji ya mwenzao.

Pamoja na mambo mengine, waandishi walilitaka jeshi hilo lirejeshe vitendea kazi vilivyokuwa vikimilikiwa na Mwangosi, ikiwamo kamera, kompyuta (laptop) pamoja na simu ya mkononi, alivyokuwa navyo wakati akiwa mikononi mwa askari polisi zaidi ya wanane kabla ya kuuawa.

Kadhalika, Mkuu wa Jeshi Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, pamoja na maofisa wengine waandamizi wa jeshi hilo, walikutana na viongozi wa Chadema na kuzungumzia hali ya baadaye baada ya kutokea kwa mauaji hayo.

Vilevile, Waziri Nchimbi aliunda kamati inayoongozwa na Jaji Stephen Ihema ili kumsaidia pia kupata majibu ya maswali, ambayo hana majibu yake kuhusiana na kifo hicho.

DK. NCHIMBI ATANGAZA TAARIFA YA AWALI YA UCHUNGUZI

Jana Waziri Nchimbi alithibitisha kukabidhiwa taarifa ya awali ya uchunguzi wa polisi juu ya mauaji ya Mwangosi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Waziri Nchimbi alisema uchunguzi huo wa awali ulibaini mambo makubwa mawili; la kwanza likieleza kuwa mlipuko uliotokea, uliotokana na bomu na la pili, bomu hilo lilifyatuliwa na askari huyo.

Waziri Nchimbi alisema katika taarifa hiyo iliyosainiwa naye kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo kutoka kwa IGP Mwema, alimweleza Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi kuwa aipeleke kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili afanye uamuzi wa kisheria juu ya uchunguzi huo.

Alisema juzi mwendesha mashtaka alikamilisha kulisoma jalada la uchunguzi huo na kuandaa mashtaka dhidi ya askari huyo.

Waziri Nchimbi alisema juzi hiyo hiyo aliliagiza Jeshi la Polisi kumpeleka mahakamani kama ilivyotakiwa na DPP.

Hata hivyo, alisema kamati aliyoiunda chini ya Jaji Ihema itaendelea na kazi yake ili kupata suluhisho la kudumu la migongano ya kikazi kati ya polisi na waandishi wa habari na polisi na vyama vya siasa na kuboresha uhusiano kati ya polisi na raia.

“Wakati mkondo wa sheria umeanza kufuatwa, nawaomba wadau wote kutoa nafasi kwa utaratibu huo wa kisheria kufanya kazi. Wizara yangu na mimi mwenywe tutaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika jitihada za kujenga taifa bora,” alisema Dk. Nchimbi.

WAANDISHI MTWARA WAANDAMANA

Waandishi wa habari mkoani Mtwara jana waliungana na wenzao kuandamana kulaani na kupinga mauaji ya Mwangosi.

Maandamano hao yaliyofanyika kimya kimya, yalianza katika Mtaa wa Bima na kuishia Ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani humo (MTPC), huku waandamanaji wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Yalipokelewa na Mwenyekiti wa MTPC, Hassan Simba, ambaye alisema wanalitazama jeshi la polisi kama mdau anayetia shaka.

MOROGORO WAANDAMANA

Mkoani Morogoro, waandishi wa habari pia walifanya maandamano kama hayo.

Maandamano hayo yalianzia katika mzunguko wa Posta katikati ya mji wa Morogoro na kwenda mpaka katika mzunguko wa kwenda Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Yalipokelewa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa huo (MOROPC), Aziz Msuya, katika maeneo ya Shani. Waandamanaji walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Akipokea maandamano hayo, Msuya alisema kifo cha Mwangosi kimewafanya waandishi wa habari kutokuwa na imani na polisi na kwamba, hakiwezi kusahaulika katika tasnia ya habari kwani kimeonyesha dhahiri kuwa polisi ni wauaji.

Aliwataka waandishi wa habari mkoani hapa kutoandika habari zozote za jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja mpaka hapo kamati ya uchunguzi itakapotoa ripoti yake.

Aliwataka waandishi wa habari kuwa waangalifu kwani kwa sasa hawako katika mazingira rafiki na jeshi hilo na kuwataka kukemea kwa nguvu zote vitendo kama hivyo isiwe kwa waandishi tu hata kwa raia.

MBEYA WAPINGA KAMATI YA NCHIMBI

Chama cha Wandishi wa Habari mkoani Mbeya (MBPC) kimesema kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi haihitajiki kwa kuwa ushahidi uliopo unajitosheleza.

Mwenyekiti wa MBPC, Christopher Nyenyembe, alisema hayo wakati akipokea maandamano ya waandishi wa habari yaliyofanyika jijini humo kwa lengo la kulaani na kupinga mauaji ya marehemu Mwangosi.

Alisema mazingira ya tukio la mauaji ya Mwangosi pamoja na picha zilizopigwa na waandishi wa habari katika eneo la tukio zinathibitisha bila kuacha shaka kuwa waliohusika kwenye mauaji hayo ni askari wa Jeshi la Polisi, hivyo kinachotakiwa kufanyika ni kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa hao badala ya kuendelea kutumia fedha za walipakodi kwa kuunda kamati ya uchunguzi.

Alisema msimamo wa MBPC wa kutofanya kazi na Jeshi la Polisi upo pale pale mpaka hapo jeshi hilo litakapojisahihisha na kuwahakikishia waandishi wa habari ulinzi na usalama wanapokuwa kazini.

Alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha Waziri Nchimbi, IGP Mwema na Kamanda Kamuhanda, kutokana na uzembe uliosababisha mauaji ya raia kwenye mikutano ya vyama vya siasa, akiwamo marehemu Mwangosi.

Imeandikwa na Vicky Macha, Iringa; Mariam Maregesi, Mtwara; Idda Mushi, Morogoro; Emmanuel Lengwa, Mbeya na Muhibu Said, Dar.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...