Saturday, August 4, 2012

WALIMU WAREJEA MZIGONI KWA MARA NYINGINE TENA



Rais wa Chama cha Walimu Tanzania CWT, Gratian Mukoba.

CHAMA Cha Walimu Tanzania-CWT-kimetangaza kusitisha rasmi mgomo wa walimu na hivyo kuwataka walimu wote nchini kurejea kazini mara moja kuanzia leo ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku kama kawaida.
Akitoa tamko la CWT kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kukiagiza Chama hicho kitoe maelekezo kwa wanachama wake kurudi kazini, Rais wa Chama hicho, Gratian Mukoba, amesema walimu wanarudi kazini huku wakiwa wamekata tamaa kutokana na hukumu hiyo.
Aidha Mukoba, amefafanua kuwa walimu wanaporudi kazini bila kuwa na mawazo yaliyotulia, utendaji wao utaathirika kwa namna moja au nyingine, hivyo Chama kinatoa wito kwa Serikali kukutana na CWT kwa haraka ili kuendeleza majadiliano ya Madai mapya ya Walimu.
Kuhusu kulipa fidia ya hasara waliyoipata wanafunzi, iliyotolewa na Mahakama, Chama hicho kimesema kinasubiri taarifa rasmi ya Serikali kuhusu hasara hiyo kwa kuwa hakina uwezo wa kufahamu hasara waliyoipata wanafunzi nchini nzima.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mukoba, wenye uwezo wa kuwasilisha hasara hiyo ni mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Serikali.
Hapo jana Chama hicho kilipongeza kauli ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa kwa kusema Serikali inajali na kuthamini mchango wa Walimu nchini.
Habari: Sufianimafoto Blog

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...