Thursday, August 30, 2012

TWITE ATUA YANGA, MAMIA WAMLAKI, SIMBA HAWAKUONEKANA


Twite baada ya kutua Uwanja wa ndege akiwa na viongozi wa Yanga

BEKI mpya wa Yanga, Mbuyu Twite ametua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere na kulakiwa na mamia ya wapenzi wa klabu hiyo, kabla ya kupakiwa kwenye gari kuelekea makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Hakuna kiongozi yeyote wa Simba wala askari polisi aliyemsogelea kama ambavyo kulikuwa kuna tishio kwamba akitua tu beki huyo wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) watamkamata kwa tuhuma za kuwatapeli dola za Kimarekani 30,000.
Inadaiwa, kabla ya kusaini Yanga, Twite aliyekuwa akichezea APR ya Rwanda alisaini Simba na kuchukua dola 30,000.
Hata hivyo, baadaye mchezaji huyo alighairi na kuamua kwenda Yanga na kurudisha fedha za Simba kupitia viongozi wa APR na St Eloi Lupopo ya DRC, ambazo zilikuwa zinammiliki kwa pamoja mchezaji huyo.
Lakini viongozi wa Simba waligoma kupokea fedha hizo ingawa viongozi wa APR na Lupopo walifika hadi ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaka kuzikabidhi fedha hizo, ili Simba wakazichukulie hapo.
Twite aliianza kuichezea Yanga wiki iliyopita ilipokuwa Kigali, Rwanda kwa ziara ya wiki moja lakini alishindwa kurejea na wenzake Jumatatu kwa kile kilichoelezwa anakamilisha kuhama kwake rasmi na kuja kuanza maisha mapya Dar es Salaam,
Lakini upande wa pili, Simba SC waliamini beki huyo amekwepa kukamatwa kufuatia kuvuja kwa habari za mpango wa kumtegea akitua nchini wamkamate.
Ametua na amekwenda Jangwani, maana yake jaribio la kumkamata akitua limefeli na sasa tusubiri kama Simba watamuwekea mtego mwingine.
Shabiki wa Yanga Babu Ally, akiwa na jezi ya Rage na4
Twite akizungumza na Waandishi huku amevaa jezi namba 4 yenye jina Rage






Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Yanga, Francis Kifukwe kushoto akiwa Uwanja wa Ndege na kigogo wa Usajili, Seif Ahmad 'Magari'


No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...