Monday, August 6, 2012

TIMU YA YANGA YAPOKELEWA KWA SHANGWE BUNGENI


 Kocha wa Timu ya Yanga, Mbelgiji Tom Saintief (mbele kulia) akifuatilia shughuli za bunge leo wakati yeye na wachezaji wake (nyuma) walipotinga 'mjengoni' kulionyesha kwa wabunge mjini Dodoma Kombe la Kagame walilotwaa kwa mara ya pili mfululizo. Yanga wamekwenda bungeni baada ya kualikwa na wabunge walio wanachama wa Yanga.  
 
KIKOSI cha klabu ya Yanga kimetua kwa kishindo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo na kuibua shangwe na nderemo kutoka kwa wabunge mashabiki wa timu hiyo wakati wakitambulisha kombe walilotwaa hivi karibuni la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame. Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wachezaji wa Yanga walioongozana na mwenyekiti Yusuf Manji, Makamu MwenyekitiClement Sanga, mjumbe wa bodi ya wadhamini, Mama Fatma Karume na Francis Kifukwe walitambulishwa na bungeni na kupongezwa na Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda. Kufuatia tukio hilo, wabunge waliripuka kwa shangwe na bashasha tele, huku wale ambao wanafahamika kuwa ni mashabiki wa Simba, kama Mhe. Ismail Aden Rage ambaye pia ni mwenyekiti wa wekundu hao wa Msimbazi, wakionekana kushangilia vilevile, lakini kwa namna ya utani zaidi. Baada ya utambulisho wa msafara wa wachezaji wa Yanga, wakiwamo nyota kama Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Hamis Kiiza na mfungaji bora wa michuano ya Kagame, Said Bahanunzi, likaja tukio la kuonyeshwa kwa kombe walilotwaa, la Kagame. Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisimama na kombe hilo, akaenda mbele na kulipunga hewani huku akilielekeza kila upande ili wabunge wote wapate nafasi ya kuliona. Ushangiliaji wa kupiga meza ulitwaa nafasi na kuufanya ukumbi mzima urindime.
Hata hivyo, katikati ya kushangilia huko, wabunge wengi ambao ni mashabiki wa Simba, wakiongozwa na Rage, wakajibu mapigo ya wapinzani wao wa jadi kwa namna ya kuchekesha zaidi baada ya kunyoosha juu vidole vitano vya mkono; pengine wakikumbushia matokeo ya kichapo kikali cha mabao 5-0 walichowapiga Yanga katika mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara! Baadaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe akawapongeza Yangawakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha. Membe ambaye pia ni mnazi wa Yanga, akasema kwamba atakuwa hajatenda haki kama hatawapongeza Yanga ambao wamekuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa Kagame unaohusisha klabu bingwa za Afrika Mashariki na Kati; na kwamba amefurahi kuwa ujio wao bungeni umekuja katika siku mwafaka ambayo wizara yake inawasilisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha. Yanga walitwaa kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo baada ya kushinda 2-0 katika mechi yao ya fainali dhidi ya Azam FC.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...