Saturday, August 4, 2012

MASHINE MPYA YATUA YANGA



Mshambuliaji mpya wa klabu ya Yanga SC, kutoka nchini Burundi Didier Kavumbangu katika picha

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu amewasili jana usiku kujiunga na klabu yake mpya, Yanga SC ya Dar es Salaam, akitokea Atletico ya Burundi.
Kavumbangu anatarajiwa kuanza mazoezi leo jioni na wenzake, kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Yanga, ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, walianza maandalizi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana na Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mbelgiji Tom Saintefiet aliwataja wachezaji ambao hawakufika jana kuwa ni Hamisi Kiiza, ambaye ameitwa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, Ibrahim Job na David Luhende ambao bado wapo kwao Mwanza, wakati Juma Abdul bado ni majeruhi.
Tom alisema wachezaji wengine waliokosekana mazoezini jana ni wale ambao wapo timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, Frank Damayo, Omega Seme na Simon Msuva.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Jumamosi kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wafungaji Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hilo lilikuwa taji la tano la michuano hiyo kwa Yanga kihistoria, baada ya awali kutwaa mataji ya Kombe hilo katika miaka ya 1975 Zanzibar, 1993, 1999 Uganda na 2011 Dar es Salaam na mara zote hizo, ikiwa chini ya makocha wa kigeni.
Mwaka 1975 Yanga ilibeba Kombe hilo, ikiwa chini ya kocha kutoka Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo (DRC), Tambwe Leya (sasa marehemu), 1993 chini ya kocha kutoka Burundi, Nzoyisaba Tauzany pia marehemu, 1999 chini ya Raoul Shungu kutoka DRC na mwaka jana chini ya Mganda Sam Timbe.
Wiki hii ziliibuka habari kwamba, baada ya kuipa Yanga Kombe la Kagame,Tom ameomba kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, lakini mwenyewe alisema baadaye akizungumza na BIN ZUBEIRY kwamba tangu amejiunga na klabu hiyo mwezi uliopita hajawahi kuomba kazi sehemu nyingine yoyote.
Mtakatifu Tom alisema anashangazwa mno na habari hizo za kizushi, za kizandiki zenye kulenga kumchonganisha yeye na mwajiri wake, Yanga SC.
“Nakumbuka niliwahi kuomba kazi Chama cha Soka Kenya (KFF) kufundisha timu yao ya taifa (Harambee Strars), lakini ilikuwa ni muda mrefu sana hata kabla sijaomba kazi Yanga,”alisema.
Blog moja iliyowahi kuandika Iddi Kipingu anagombea Uenyekiti Yanga, wiki hii iliandika habari yenye kichwa kisemacho; “WIKI MOJA BAADA YA KUIPA UBINGWA: KOCHA WA YANGA TOM SAINTFIET ATUMA MAOMBI YA KUIFUNDISHA HARAMBEE STARS,”. Akiizungumzia habari hiyo, Mtakatifu alisema; “Ni uongo, tangu nimesaini mkataba na Yanga, sijawahi kuomba kazi pengine popote,”alisema.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...