Thursday, July 26, 2012

YANGA, AZAM KATIKA MTIHANI MZITO WA KUBAKIZA KOMBE NYUMBANI LEO



Spider Man
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC leo wanashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na timu ya Jeshi la Rwanda, APR katika Nusu Fainali ya pili ya michuano hiyo kuanzia saa 10:00 jioni, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu Fainali ya kwanza kati ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Azam FC.
Yanga iliingia Nusu Fainali baada ya kuitoa Mafunzo ya Zanzibar kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, wakati APR iliitoa URA ya Uganda kwa kuichapa mabao 2-1.
Nusu Fainali ya pili inayozikutanisha Azam FC iliyoitoa Simba kwa kuichapa 3-1 na AS Vita iliyoitoa Atletico ya Burundi kwa kuichapa 2-1, itaanza saa 8:00 mchana Uwanja huo huo wa Taifa.
Azam na Vita nayo itakuwa mechi tamu, kwa sababu timu zote zinacheza soka ya kuvutia na zina wachezaji wenye vipaji- zaidi kila timu ina mshambuliaji anayewania ufungaji bora wa michuano hii.
Azam kuna John Raphael Bocco ‘Adebayor’ mwenye mabao manne akifungana na Hamisi Kiiza wa Yanga katika nafasi ya tatu, wakati Vita inaye kinara wa mabao katika Kagame ya 2012, Etikiama Taddy mwenye mabao sita, akifuatiwa na Said Bahanuzi ‘Spider Man’ wa Yanga mwenye mabao sita.
Akizungumzia mchezo dhidi ya APR, kocha wa Yanga, Tom Saintefiet alisema kwamba utakuwa mgumu kwa sababu timu hizo zitakuwa zinakutana mara ya pili, baada ya mechi ya awali ya kwenye Kundi lao, C ambayo Yanga ilishinda 2-0.
“Utakuwa mchezo mgumu, APR ni timu nzuri, wanacheza kwa ufundi, nguvu, lakini tunataka kushinda na tutakwenda kupigana ili kushinda,”alisema Tom.


John Bocco 'Adebayor'

Hata hivyo, Mbelgiji huyo alisema katika mchezo wa leo atawakosa kipa wake namba moja Yaw Berko na kiungo Nizar Khalfan ambao wote ni majeruhi.
Mtakatifu Tom alisema kutokana na kucheza mechi mfululizo, wachezaji wengi wa Yanga wanalalamika maumivu, ila wako tayari kucheza na wana nia na dhamira ya kutetea Kombe.
Safu ya ushambuliaji ya APR inaweza kuongozwa na wakali wawili, Mrundi Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi ambao wote wana miili mikubwa ni hatari kweli sambamba na kiungo mshambuliaji, Mganda Danny Wagaluka, wakati Yanga bila shaka Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza wataendelea kumpumzisha kwenye benchi Jerry Tegete na Haruna Niyonzima ataongoza safu ya kiungo.
Kihistoria mechi kati ya Yanga na APR huwa ni kali na za kusisimua tangu zianze kukutana mwaka 1996 katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na mara nyingi watoto wa Jangwani ‘hutoshana nguvu’ na timu hiyo ya jeshi la Rwanda.
Azam ikiwa na morali ya hali ya juu, safu yake ya kiungo inatarajiwa kuongozwa na kiungo bora mzalendo kwa sasa Tanzania, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’ wakati kwenye ushambuliaji mfungaji bora wa Ligi Kuu, Adebayor wa Chamazi atapewa dhamana.
BIN ZUBEIRY inazitakia kila la heri timu za Tanzania katika hatua hii zishinde leo na kulihakikisha Kombe la Kagame kuendelea kuishi katika Bandari Salama. Mungu ibariki Tanzania, zibariki Azam na Yanga. Amin.


JE WAJUA?

1. Klabu ya Armee Patriotique Rwandaise, maarufu kama A.P.R., ilianzishwa mwaka 1993 na inamilikiwa na Jeshi la Rwanda na katika kipindi cha uhai wake, mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda mara 12 (1995, 1996, 1999, 2000, 2001, 2003, 2005, 2006, 2007, 2009, 2010 na 2011), Kombe la Kagame mara mbili (2004 na 2007) na kufika Nusu Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 2003.



2. Young Africans SC maarufu kama Yanga iliyoanzishwa rasmi mwaka 1935, hadi sasa mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara mara 23, (1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009 na 2011), Kombe la Kagame mara nne (1975, 1993, 1999 na 2011), kufika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara tatu (1969, 1970 na 1998) na Kombe la Washindi 1996.

3. Wakati Yanga, kocha wake ni Mbelgiji Tom Saintfiet, APR inafundishwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts- na wakati Yanga Mwenyekiti wake ni mfanyabiashara milionea, Yussuf Manji, APR Mwenyekiti wake ni mdogo wa rais wa Rwanda, Paul Kagame aitwaye Alex Kagame.

4. Nembo ya Yanga ina alama ya Mwenge, ramani ya Afrika na mpira- ikimaanisha kushiriki harakati za Uhuru wa Tanganyika, ambayo baadaye iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania (Mwenge), timu halisi ya Afrika (ramani) na timu ya mpira (mpira), wakati nembo ya APR ina alama ya mnyama Simba na mpira- vikimaanisha, ni wafalme kama mnyama Simba porini (Simba) na timu ya mpira (mpira).

5. Wakati Yanga ambayo huvalia jezi za rangi ya kijani na njano, ilishiriki michuano hii kwa mara ya kwanza mwaka 1975 na kutwaa Kombe, APR ambao huvalia jezi za rangi nyeupe na nyeusi siku zote, mara nyingi zikiwa za mistari ya punda milia, ilishiriki kwa mara ya kwanza michuano hii mwaka 1996 na kushika nafasi ya pili, baada ya kufungwa 1-0 na Simba kwenye fainali.


6. Wakati wapinzani wa jadi wa Yanga, nchini Tanzania ni Simba SC kwa APR wapinzani wao wa jadi Rwanda ni Rayon Sport.


Makocha; Ernest Brandy Mholanzi wa APR kulia na Tom Saintfiet Mbelgiji wa Yanga



REKODI YA YANGA NA APR KAGAME;
1996 Dar es Salaam; Yanga 2-2 APR (Nusu Fainali, APR ilishinda kwa penalti 4-2)
2008 Dar es Salaam; Yanga 2-2 APR (Kundi C)
2012 Dar es Salaam; Yanga 2-0 APR (Kundi C, Julai 20)
2012 Dar es Salaam; Yanga V APR (Nusu Fainali, Julai 26)

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...