Friday, June 8, 2012

MTOTO MWENYE VICHWA VIWILI AZALIWA MUHIMBILI

Mtoto wa ajabu amezaliwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akiwa na vichwa viwili, lakini kiwiliwili chake kikiwa na viungo vya kawaida.
Habari zilizopatikana hospitalini hapo, zinaeleza kuwa, mtoto huyo alizaliwa usiku wa kuamkia juzi akiwa na uzito wa kilo 3.5 na mwanamke mmoja ambaye jina lake limekuwa siri.
Taarifa hizo zilisema kuwa, mara baada ya mtoto huyo kuzaliwa, wakunga waliokuwa wakimzalisha mwanamke huyo walishangaa kuona mtoto huyo akiwa na vichwa viwili vilivyoungana katika kiwiliwili cha mwili mmoja.
Mmoja wa wauguzi hospitalini hapo aliliambia NIPASHE kuwa, mtoto huyo mara baada ya kuzaliwa alipelekwa haraka katika chumba maalum kwa ajili ya uchunguzi.
“Kwa kweli haijafahamika mara moja kama yule mtoto ana uwezo wa kunyonya ama la, kwani wameungana shingoni wakati miguu na mikono ikiwa miwili miwili,” alisema muuguzi huyo kwa sharti la kutotaja jina lake.
Hata hivyo, mfanyakazi mwingine wa hospitali hiyo alisema juhudi zinafanywa na madaktari bingwa wa hospitali hiyo kuchunguza kwa kutumia mashine maalum kama vichwa hivyo vinachangia moyo mmoja.
“Madaktari wapo katika harakati za kumfanyia uchunguzi kuangalia kama wanachangia moyo kwa ajili ya kuangalia njia sahihi ya kuokoa maisha angalau ya mtoto mmoja,” aliongeza.
Aidha, habari kutoka ndani ya hospitali hiyo zinaeleza kuwa uongozi wa hospitali umewazuia watu kwenda kumuona mtoto huyo baada ya kutokea tukio la kuzirai kwa mmoja wa wanafamilia hiyo aliyekwenda kumuona.
Afisa Uhusiano Msaidizi wa Muhimbili, Jezza Waziri, alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema bado imekuwa mapema kuelezea tukio hilo kwa sababu kuna hatua mbalimbali zinachukuliwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi.
“Sina la kuongea kuhusu tukio hilo, subiri kwanza tufanye mawasiliano na viongozi wangu na kama ikihitajika kutolewa nitawaambia,” alisema Waziri.

TUKIO KAMA HILI NCHINI
Matukio kama hayo yamewahi kutokea nchini kwa mfano, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Devotha Ernesta, mkazi wa Msowero wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, alijifungua watoto wa mapacha walioungana kuanzia sehemu ya kichwa mpaka kiwiliwili wakiwa na miguu minne na mikono minne.
Tukio hilo lilitokea Mei 8, mwaka huu kwenye Hospitali ya Wilaya Kilosa, baada ya mwanamke huyo kufika hospitalini hapo akiwa na ujauzito uliokamilika siku za kujifungua.
Muda ulipofika ndipo alipojifungua watototo walioungana wakiwa na uzito wa kilo nne, lakini muda mfupi baada ya kuzaliwa walifariki dunia.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Moses Mwemsanga, alisema kuzaliwa kwa watoto hao ni hali ya kawaida inayoweza kutokea kwa mtu yeyote na kwamba kunasababishwa na mbegu za kike na za kiume kuungana na baadaye kushindwa kugawanyika.
Alisema kuwa watoto hao walikuwa mapacha, lakini ilishindikana kugawanyika baada ya mbegu za mwanamke na mwanaume kuungana na kuongeza kuwa ni hali ya kawaida ambayo inaweza kutokea kwa mtu yeyote ingawa hutokea kwa nadra sana.
Mwanamke aliyejifungua watoto hao, Devotha Ernest, alisema katika maisha yake hakuwahi kuona mtoto kama huyo aliyejifungua na hawezi kuhusisha na imani za kishirikina bali ni mapenzi ya Mungu.
Devota alisema alikuwa anatamani sana ajifungue salama apate furaha na mtoto wake, lakini mwenyezi Mungu ameamua kutekeleza alichokusudia kwa mapenzi yake na hawezi kuhusisha na tukio la kishirikina kutokana na kujifungua mtoto huyo.
Tukio la pili lilitokea Zanzibar Januari 1, 2010, ambapo mwanamke mkazi wa mjini Zanzibar, Farihati Maulid (18), alijifungua watoto mapacha walioungana.
Mwanamke huyo alijifungua kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Mapacha hao walikuwa wa kiume ambao waliungana wakiwa na moyo mmoja na waliunganika kuanzia kwenye kitovu hadi kwenye mfupa wa kidari huku wakiwa na uzito wa kilo 2.8.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...