KAPOMBE AFURAHIA TUZO, LAKINI...
Kapombe kushoto, akipokea tuzo ya Mwanamichezo Bora, kutoka kwa Salim Amir mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania. Anayeshuhudia katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu'.
Kapombe kushoto, akipokea tuzo ya Mwanamichezo Bora, kutoka kwa Salim Amir mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania. Anayeshuhudia katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu'.
KIUNGO chipukizi wa Simba SC, Shomary Kapombe amesema kwamba mafanikio anayoyapata hivi sasa ni changamoto nzuri kwake na hatalewa sifa, badala yake ataongeza juhudi ili afike mbali kisoka.
Akizungumza usiku wa jana katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Kapombe alisema kwamba amefurahi mno kutwaa tuzo mbili, Mwanamichezo Bora Anayechipukia na Mwanamichezo Bora wa Jumla wa mwaka Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), lakini hatalewa sifa.
“Nimefurahi kwa kweli, ila kwangu hii ni kama changamoto na ninawaahidi Watanzania kwamba sitalewa sifa na nitajitahidi nifike mbali,”alisema Kapombe.
Kiungo huyo anayeweza kucheza kama beki wa kati na kulia pia, alisema kwamba ndoto zake kwa sasa ni akitoka Simba akacheze Ulaya na kulingana na mafanikio yake ya sasa akiwa bado mdogo Kapombe alisema anaamini atatimiza ndoto zake.
“Naamini nitafika mbali, kwa sababu siri ya mafanikio ya mchezaji ni bidii ya mazoezi na kusikiliza mafundisho ya walimu wake, nami nitazingatia hilo,”alisema mfungaji huyo wa bao la kusawazisha katika ushindi wa 2-1 wa Tanzania dhidi ya Gambia Jumapili, ikitoka nyuma kwa 1-0 katika mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia 2014.
Kapombe amemaliza msimu mmoja tu Simba SC tangu asajiliwe kutoka Polisi ya Morogoro, lakini kwa sasa tayari ni tegemeo la klabu yake na timu ya taifa. Kijana anacheza kwa bidii na ana kipaji, kiasi kwamba hata kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen anamtabiria kufika mbali.
“Kapombe ni kati ya wachezaji wangu ambao nina matumaini watafika mbali, namtakia kila heri na nampongeza kwa mafanikio yake,”alisema Poulsen usiku wa jana.
Pamoja na kukesha Diamond Jubilee usiku wa jana, lakini Kapombe ameondoka na kikosi cha Taifa Stars alfajiri ya leo kwenda Msumbiji kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini dhidi ya wenyeji Jumapili, Tanzania ikitakiwa kushinda au sare ya mabao yasiyopungua 2-2 ili isonge mbele, kufuatia awali kulazimishwa sare ya 1-1.
No comments:
Post a Comment