Wednesday, June 6, 2012



MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema moto uliowashwa na chama hicho katika Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, lengo likiwa ni kuiondoa CCM madarakani na iwapo itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu siasa.

Mbowe alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakati chama hicho kilipofanya mkutano mkubwa kwenye uwanja wa mpira wilayani humo.
Alisema CCM kimepoteza mwelekeo wa kuongoza taifa na ndiyo sababu maisha ya Watanzania yamezidi kuwa mgumu kadri miaka inavyozidi kusonga mbele.

“Wajibu wa Serikali kokote duniani ni moja tu, kuwezesha watu wake kutoka katika hali ngumu za maisha na kuwapeleka kwenye heri, leo CCM wameligawa Taifa katika vipande, wanauza rasilimali za nchi na kuwadidimiza watu wa kipato cha chini wengi wao wakiwa ni wakulima,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Ndugu zangu ngojeni niwaulize swali, wakati wa utawala wa Mwinyi na Mkapa (marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa), ni kipindi gani maisha yalikuwa mazuri?” Wananchi wakajibu (kipindi cha Mwinyi). Miaka 10 ya uongozi wa Mkapa na miaka saba ya Kikwete, ni kipindi gani maisha yamekuwa magumu zaidi?" Wakajibu (Kikwete); Je, 2015 wanakuja tena kutuomba kura huyo atakayekuja si ndiyo itakuwa mbaya zaidi, Chadema hatuwezi kukubali na moto huu tuliowasha utaendelea nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kama CCM itasalimika nitajiuzulu siasa.”

Mbowe alikishambulia CCM akidai kimepoteza mwelekeo uliowekwa na waasisi wake, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere wa kuzingatia usawa, udugu huku kikijikita katika msingi wa kutetea wakulima wanyonge na wafanyakazi lakini sasa kimewagawa wananchi katika matabaka ya walio nacho na wasio nacho.

“CCM ya Mwalimu Nyerere ilijali wakulima na wafanyakazi wa kipato cha chini, ilijenga mshikamano baina ya Watanzania wote bila kujali ukabila. Tanzania ina makabila zaidi ya 120, lakini tunaishi kama mtu na ndugu yake, leo taifa limegawanyika vipande huku maadili ya uongozi yakiporomoka,” alisema Mbowe.

Katika mkutano huo uliokutanisha viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho, Mbowe alisema kwa sasa CCM kimevuruga hata mitalaa ya elimu huku akituhumu watunga sera kuwa wanafanya hivyo makusudi kwa kuwa watoto wao hawasomi katika shule hizo.

“Mwalimu alijenga CCM iliyozingatia usawa, watoto wote walisoma shule moja, mimi nilisoma na watoto wa Mwalimu Nyerere, mawaziri na wakulima katika shule hiyo, leo watoto wa mkulima wanasoma shule za kata ambazo hazina walimu, vitabu, maabara wala library (maktaba), wakati watoto wa vigogo wakisoma nchi nje na wale wa wakuu wa wilaya wakisoma shule za (academy),” alisema Mbowe.
Aliwataka wakazi wa mikoa ya kusini, Lindi na Mtwara kuunganisha nguvu kwa lengo la kukiondoa CCM madarakani katika chaguzi zote ukiwamo mkuu wa 2015.

“Ndugu zangu wa Masasi, mimi Mbowe ninatimiza miaka 21 nikiongoza siasa za upinzani zenye lengo la kuleta ukombozi wa kweli kwa Taifa hili, nimefunguliwa kesi za uchochezi tisa hadi leo, lakini sitaacha harakati hata wakinifunga, bado nitaendelea na harakati za ukombozi hadi Watanzania watakapofikia kwenye uhuru wa kweli,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alieleza kusikitishwa kwake na umaskini unaoukabili Mkoa wa Mtwara licha ya kuwapo rasilimali nyingi zinazouzunguka ikiwamo gesi na korosho.

Alisema kumekuwa na ufisadi mkubwa unaofanywa katika ununuzi wa korosho na licha ya wananchi kukatwa Sh30 katika kila kilo wanayouza, bado mikoa hiyo ya kusini inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, huduma muhimu za kijamii kama zahanati na shule.

“Taifa linaweza kuendelea ikiwa rasilimali za nchi ambazo zinatoka kwa wananchi zitawarudia na kutumika katika kuendeleza miradi ya maendeleo. Leo mnakatwa Sh30 katika kila kilo moja ya korosho mnayouza, tumetafuta ni kiasi gani cha korosho kimepatikana kwa mwaka hapa nchini lakini taarifa hizo hatuzipati.”

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...