TAMKO LA ASKOFU MKUU WA TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD, DK.BARNABAS
MTOKAMBALI, KUHUSU MATUKIO YANAYOASHIRIA UVUNJIFU WA AMANI NCHINI.
Kwa
kipindi kirefu sasa kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayoashiria
uvunjifu wa amani, umoja na utengamano wa taifa letu la Tanzania, haya
ndiyo yanayonisukuma kutoa tamko hili leo ili kuonya na kushauri.
Katika siku za karibu kiumeibuka makundi mbalimbali ya kidini ambayo
yalianza kutoa matamko yenye kuchochea ghasia za kidini Tanzania, na
pengine kauli hizo ndizo zinazotimizwa kwa vitendo hivi sasa.
Miongoni mwa matukio hayo ni: Januari sita mwaka huu, kikundi kimoja kinachoitwa JUAKATA, kiliitisha
kongamano
la kujadili katiba mpya Tanzania, kwa upande wa Waislam. Katika
kongamano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee,Dar es
Salaam kauli zifuatazo:
1. Lazima Rais ajaye atoke Zanzibar
2. Kukabiliana na ukuaji wa kasi wa dini ya Kikristo
3. Kupinga Muungano ili kuupa nguvu Uislamu
4. Kupigana kufa na kupona kutetea maslahi yao wakati huu wa kuandaa
katiba
mpya. Kauli hizo zilitolewa na Sheikh Nasor Mohameed, kutoka Zanzibar,
ambaye alikuwa mgeni rasmi. Baadaye zikaandaliwa kanda za CD
zilizosambaza ujumbe huo.
Uchunguzi unaonesha kuwa miongoni mwa
makanisa yaliyochomwa hivi karibuni huko Zanzibar ni ya EAGT, Elimu
Pentecost na TAG, Anglikana, Katoliki na FPCT, hivyo kujenga taswira ya
ubaguzi wa kidini ambao kama hautapatiwa dawa unaweza kuligawa taifa la
Tanzania kamailivyotokea Nigeria na kwingineko barani Afrika.
Hofu yangu ni kuwa, roho hii ya ubaguzi wa kidini ambayo Baba wa Taifa
hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliifananisha na dhambi ya kula
nyama ya mtu, imekuwa ikiyatafuna mataifa ya Afrika kama ifuatavyo:
1. Mwaka 2000, vuguvugu la kuanzishwa kwa utawala wa Kiislamu (Sharia),
lilianza kwenye majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria, miaka michache
baadaye majimbo kadhaa yakajitangazia sheria hizo na tangu wakati huo
kumekuwa na mapambano yasiyoisha. Takwimu zinaonesha kuwa
katika miaka ya karibuni zaidi ya Wakristo 500 wameuawa kikatili na makanisa kuchomwa moto.
2.
Roho hii imekuwa ikienea kwa kasi katika maeneo mbali mbali ya Afrika
ambapo imelikumba taifa la Mali, majimbo ya kaskazini tayari yametangaza
kujitenga na kuna vuguvugu lenye kuhusisha mapigano ya silaha.
3. Itakumbukwa kuwa wiki chache tu zilizopita vuguvugu hili la kudai
utawala wa kidini liliibuka nchini Kenya ambapo watu wanaojiita
wanaharakati walianzisha madai ya kutaka eneo la Pwani kujitenga na
Jamhuri ya Kenya na kujitangazia taifa la Kiislamu.
4. Ni wakati
huu ambao kundi la Uamsho linalopinga kuandikwa kwa katiba mpya kabla
ya kuitishwa kwa kura ya maoni ili wanzazibar waamue kuhusu Muungano
liliibuka na kuanzisha ghasia Zanzibar ambazo zimepelekea makanisa
kadhaa kuchomwa moto na mali kuharibiwa, huku watu wa bara wakitishiwa
maisha.
USHAURI WANGU KWA SERIKALI NA VIONGOZI WA DINI
Ni wajibu wa kila Mtanzania kutii sheria na mamlaka kwa kuwa zimewekwa
kuruhusiwa na Mungu, hivyo kuziasi ni Kumuasi Mungu, yaani ni dhambi.
Hivyo kila Mtanzania anastahili kukumbuka wajibu wake wa kutii mamlaka.
Viongozi wenzangu wa dini wakumbuke kuwa wana wajibu mkubwa katika
jamii, na jamii inawasikiliza hivyo ni vyema wakawa makini katika
matamshi na maelekezo yao ili wasiwe chanzo cha kuchochea vurugu za
kidini na uvunjaji wa amani.
Ni vyema wakati huu wa kuandikwa
kwa katiba mpya, kila kikundi kikafuata utaratibu uliowekwa badala ya
kuchochea ghasia ambazo madhara yake yatawakumba watanzania wote ikiwa
ni pamoja na wao wenyewe watoto na wajukuu zao.
Pia ningependa
kuwashauri viongozi wa serikali kusimama imara katika kusimamia sheria
na haki, na kuepuka kauli au vitendo vitakavyofanya baadhi ya watanzania
kudhani kuwa hawatendewi haki.
Ni vema ieleweke kuwa matukio
kama haya ya uvunjaji wa amani yasipodhibitiwa na kukomeshwa haraka
yanaweza kuumba chuki ambayo inaweza kuibua mlipuko mkubwa na machungu
kwa wananchi na matokeo yake yakawa mabaya kwa Taifa zima. Hekima na
busara inatufundisha kuwa tusipoziba ufa tutajenga ukuta.
Ni
vyema wenye dhamana ya kuongoza wakakumbuka kuwa wanawajibu mbele ya
Mungu aliyewaweka au kuwaruhusu kuingia madarakani na siku moja watatoa
hesabu mbele zake.
Mwisho, natoa wito kwa watanzania wenzangu
tuulinde umoja, amani na utengamano wa taifa letu, tuikimbie dhambi ya
ubaguzi kwa kuwa tukiiruhusu itatuangamiza sote. Tuliombee taifa letu na
kukiwa na mbegu ya chuki tuimalize kwa njia ya majadiliano na vikao vya
pamoja vinavyohusisha viongozi wa dini zote na serikali pia.
Imetolewa leo 28/05/2012
Na Dk. Barnabas Mtokambali
Askofu Mkuu wa TAG
No comments:
Post a Comment