Wednesday, May 23, 2012

SIMBA YASAJILI KIUNGO MKENYA KWA MIL.9

Na Mwandishi Wetu
NAHODHA wa Klabu ya FC Leopards ya Kenya, Salim Kinje, anajiandaa kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba kwa ada ya zaidi ya Sh milioni 90.
Kiungo huyo ambaye ni raia wa Tanzania, anatua Simba baada ya kuwindwa kwa muda mrefu na timu iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi kuu msimu uliopita, Azam FC.
Mtandao wa SuperSport.com umesema kuwa mchezaji huyo ambaye amezivutia klabu nyingi za Tanzania, ataondoka na kujiunga na Simba kwenye usajili wa mwezi ujao.
Imefahamika kuwa sababu kubwa ya mchezaji huyo kujiunga na Simba ni kuweza kupata nafasi ya kukichezea kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Kocha wa Leopards, Jan Koops, amethibitisha kuondoka kwa mchezaji huyo na kusema hataendelea tena kuitumikia timu hiyo.
“Kinje aliniita na kuniambia kuwa amepata ofa nzuri kwenye kikosi cha Simba na anataka kuondoka. Huyu ni Mtanzania na anataka kwenda kucheza soka nchini kwao.
“Tutammisi sana, alikuwa kiongozi mzuri wa wachezaji wetu, alikuwa nahodha wa pili wa timu na hili ni pigo kubwa sana kumpoteza.”
Taarifa kutoka kwenye Mtandao wa Ingwefans wa Kenya, zinasema kuwa Simba inamsajili kiungo huyo kwa kitita cha shilingi za Kenya milioni 5 ambazo ni zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni 90.
Mtandao huo umeendelea kueleza kuwa kiungo huyo anatarajiwa kutoka Kenya leo ili kuja kukamilisha mkataba na Wekundu hao baada ya kuwaaga wachezaji wenzake juzi.
Maoni ya mashabiki wa timu hiyo kwenye mtandao huo yalionyesha kuwa Kinje alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo kabisa wa kikosi hicho lakini wengi waliamini kuwa kitita cha fedha kilichotolewa na Simba kitaweza kuibadilisha timu hiyo.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alishindwa kukubali au kukataa. Alisema: “Tunajua kwamba Kinje ni mchezaji mzuri lakini kwa sasa hatuwezi kusema kama tutamsajili au hatutamsajili.”
CHANZO:GAZETI LA CHAMPION

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...