Thursday, March 22, 2012

BASATA YAWAFUNDA WAMILIKI WA BENDI NCHINI

Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego (kulia) akionesha kitabu cha Sera ya Taifa ya Utamaduni kwa viongozi na wamiliki wa Bendi za jijini Dar es Salaam kwenye semina iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii. Kulia ni Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa, BASATA Bi. Vivian Shalua.

Mkurugenzi wa Bendi ya African Stars Twanga Pepeta, Asha Baraka akichangia jambo wakati wa semina fupi ya viongozi na wamiliki wa Bendi za jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Bendi ya Mapacha Watatu, Khamis Dakota akizungumzia tatizo la wanenguaji kushusha nguo zao mara wanapopandwa na mizuka jukwaani. Alishauri vikundi visivyosajiliwa vifuatiliwe.

Meneja wa Ukumbi wa maonesho wa Continental wa jijini Dar es Salaam akielezea maonyesho yanayofanyika Ukumbini kwake.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii limeendesha semina kwa viongozi na wamiliki wa bendi nchini ili kusisitiza maadili na utambulisho wa Taifa miongoni mwa bendi hizo.

Akizungumza kwenye semina hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba, Katibu Mtendaji wa baraza hilo Ghonche Materego alisema kuwa, ni lazima sasa wasanii wawe kweli kioo cha jamii, wawe vielelezo na wabebe utambulisho wa mtanzania.

“Ni lazima bendi na wasanii wetu kwa ujumla wajiulize hivi kweli wao ni kioo cha jamii? Wanatoa kweli utambulisho wa mtanzania? Ni vielelezo vya mtanzania? Tukijiuliza maswali haya tutaweza kujua nini tunafanya katika kulinda utamaduni wetu” alisema Materego.
Aliongeza kuwa, wasanii hawana budi kujua jinsi ya kuitumia Sanaa kulingana na hadhira pia wakati lakini zaidi waweze kuhakiki kazi zao za Sanaa kabla ya kuzipeleka kwa walaji.

Akinukuu baadhi ya vipengele kutoka kwenye sera ya Taifa ya Utamaduni, Bw. Materego alisema kuwa, BASATA kama moja ya mtekelezaji wa sera hiyo ya utamaduni litahakikisha shughuli zote za burudani nchini hazipotoshi maadili ya taifa.

“Sera ya Utamaduni katika sura ya 9 inaeleza haja ya kuchukua hatua kali dhidi ya wasanii na vikundi vya sanaa vinavyokiuka maadili ya taifa. Tumeona tuwaite tukumbushane haya kabla hatujafikia hatua hii” alisisitiza Materego.

Aliongeza kuwa, Sanaa ni kazi na Baraza lisingependa kukatisha ajira za Wasanii lakini akasisitiza kuwa, hatua iliyofikia sasa kunahitaji mabadiliko vinginevyo hatua zitachukuliwa ili kudhibiti udhalili kwenye sekta ya Sanaa.

Kwa upande wake wamiliki na viongozi wa Bendi walisema kuwa, kumekuwa na tatizo la wanenguaji wenyewe kushusha nguo zao wanapokuwa kwenye maonyesho lakini wakaahidi kudhibiti hali hiyo.

“Ni kweli kuna tatizo hilo la uvaaji hovyo kwenye maonyesho lakini nashauri Baraza liwe na mfano wa mavazi yatakayotumiwa na wanenguaji lakini pia lifuatilie vikundi ambavyo havijasailiwa na vinafanya maonyesho yanayovuruga maadili ya taifa” alishauri Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’


No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...