Saturday, April 11, 2015

Ni Mshikemshike

Na Waandishi Wetu
SERIKALI imeyafuta maagizo yake iliyokuwa imeyatoa kwa madereva ambao jana waliitisha mgomo wa nchi nzima uliodumu kwa takribani saa saba, wakipinga utekelezaji wake.
Agizo la kufutwa kwa maagizo lilitolewa na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Gaudencia Kabaka, akiwa sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.


Akitangaza kufutwa kwa maagizo hayo, Waziri Kabaka alisema Serikali haina nia ya kuwaumiza madereva, hivyo baada ya kukutana nao na kusikiliza madai imeondoa agizo lake lililokuwa likiwataka kwenda kusoma kwa muda wa mwezi mmoja kila baada ya miaka mitatu, ambapo kisheria wanatakiwa kusajili upya leseni zao za udereva.
Wakati Waziri Kabaka akitangaza kufutwa kwa agizo hilo, Kamishna Kova yeye alitangaza kuondolewa kwa utaratibu wa kuwepo tochi zinazomulika magari yanayokwenda mwendo kasi barabarani.
Madereva hao walianza mgomo wao jana asubuhi majira ya saa 12 na kusababisha usumbufu kwa abiria waliokuwa wakisafiri ndani ya Jiji la Dar es Salaam na wale waliokuwa wakisafiri kwenda mikoani.
Mgomo huo ulimlazimu Waziri Kabaka kufika eneo la Stendi Kuu ya Ubungo kwa ajili ya kuzungumza na madereva hao na baada ya kuwasikiliza alisema madai yao si mapya kwa Serikali, lakini tatizo ni kutokuwepo kwa ufuatiliaji na utekelezaji sambamba na mikataba ya kinyonyaji wanayopewa na waajiri wao.


“Wafanyabiashara wanataka faida zaidi, hivyo mikataba waliyonayo ni geresha tu kwa ajili ya kuwaonyesha maofisa kazi wa wizara na SUMATRA.
“Ukiangalia mikataba hiyo haina makubaliano kati yao na wafanyakazi, sasa wamiliki wote wa mabasi kuanzia leo wanatakiwa kufika na kufanya usajili wakiwa na madereva wao husika wanaowaombea mikataba wakiambatanisha na picha zao,” alisema Kabaka.
Alilisitiza kuwa suala hilo ni makubaliano yaliyofikiwa na Wizara italisimamia na kuhakikisha madereva wanakuwa na maisha bora sawa na wafanyakazi wengine kwa kuondoa hali iliyopo ya kutothaminika na waajiriwa.
“Kwa kuwa haya ni mambo mazito na yanahitaji utulivu kuyatatua, nashauri Aprili 18, tukutane mawaziri wote husika, pamoja na viongozi wa madereva ili tupate ufumbuzi wa haya madai yenu,” alisema Waziri Kabaka.
Katika madai yao, madereva hao walimtaka Waziri Kabaka kufuta agizo la madereva kurudi shule kila baada ya miaka mitatu wanapokwenda kusajili upya leseni zao, kwa sababu hawana uwezo wa kumudu gharama za masomo.
Waziri Kabaka aliwaambia madereva hao kuwa agizo hilo limefutwa mpaka mikataba yao itakaposhughulikiwa na mhusika wa kulipa gharama za masomo atakuwa mwajiri.
Kamanda Kova
Naye Kamishna Kova ambaye aliambatana na Waziri Kabaka katika mazungumzo na madereva hao, alitangaza kuwa Jeshi la Polisi limefuta utaratibu wa kuyamulika tochi magari ili kubaini kama yanakwenda mwendo kasi au la na kwamba vizuizi vya magari barabarani navyo vitaondolewa.
“Kuanzia sasa hapatakuwapo na tochi wala vizuizi vya magari barabarani, pia suala la shule halipo tena tumelifuta,” alisema Kamanda Kova.
Kamanda Kova aliwasili katika Stendi ya Mabasi Ubungo majira ya 3:00 asubuhi kwa ajili ya kuzungumza na madereva hao, lakini walikataa kukutana naye mpaka Waziri Kabaka, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na Viongozi wa Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) watakapofika.
Kamanda Kova alilazimika kukubaliana na madereva hao kwa kuwasiliana na viongozi hao na baada ya muda mfupi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, alifika eneo hilo.
Waziri Kabaka alifika eneo hilo muda mfupi baadaye akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadick na kuingia moja kwa moja katika chumba walichofanyia mazungumzo na viongozi wa madereva.
Baada ya mkutano huo mfupi, Waziri Kabaka na ujumbe wake walitoka nje kwa ajili ya kisikiliza madai ya madereva ambayo yaliwasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva, Shabani Mdemu.
Madai ya madereva
Mdemu alilitaja dai la kwanza la madereva wa mabasi ya mikoani, malori na daladala kuwa wanataka kuboreshewa mikataba yao ya ajira kwa sababu kwa muda mrefu wanafanya kazi kama vibarua.
“Wamiliki wa magari wanatumia mikataba feki ya kuombea leseni kwa kuweka picha za watu wengine, huku baadhi wakitumia picha za marehemu, jambo ambalo linatunyima haki zetu nyingi,” alisema Mdemu.
Alisema kukosekana kwa mkataba kumewafanya wafanye kazi bila ya kupewa mishahara na badala yake wanapewa posho ya Sh 30,000 hadi 40,000 kwa siku, hali inayowafanya kuwa na maisha magumu, huku matajiri wakiendelea kupata faida.
Dai la pili lililowasilishwa na Mdemu ni kuondolewa kwa agizo la kwenda kusoma kila baada ya miaka mitatu, huku wakitakiwa kulipa Sh 560,000 kama gharama za masomo na kusajili upya leseni zinazokuwa zimekwisha muda wake.
Madai mengine aliyoyataja Mdemu ni madereva kukwazwa na ratiba za safari zinazotolewa na Polisi na Sumatra kwa sababu huwa zinatofautiana.
Alisema wakati Polisi wanataka dereva aendeshe kwa mwendo kasi wa spidi 80, Sumatra wanataka magari yawahi kufika.
Mkuu wa Mkoa
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alisema kuwa madai ya madereva yaliwahi kufika ofisini kwake mwaka 2013 na kufanyiwa kazi, lakini anashangaa utekelezaji wake unaonekana kukwama.
“Poleni sana madereva pamoja na abiria kwa usumbufu uliojitokeza, nilijua matatizo yenu yametatuliwa, kumbe bado wakati kipindi kile nilitoa maelekezo na nilivyoona kimya nilijua matatizo yenu yamekwisha.”
Hali ilivyokuwa awali
Shughuli za kimaendeleo katika Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo zilisimama kwa muda kutokana na mgomo huo.
Licha ya shughuli kusimama kwa muda wa saa kadhaa, ikiwemo huduma ya usafiri kwa jiji zima la Dar es Salaam na magari yaendayo mikoani na nchi jirani, lakini pia madereva wengine walilazimika kuomba nguvu ya ziada kwa kuzuia baadhi ya pikipiki na magari ambayo yalikuwa yakifanya shughuli za usafirishaji.
Wakati wa mgomo huo, madereva hao waliwasha matairi barabarani eneo la mlango wa kutokea stendi hiyo ili kuzuia magari kusafiri na ndipo polisi walipofika na kuanza kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.
Katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, baadhi ya magari yaliyokuwa yakisafirisha abiria baada ya daladala kujiunga kwenye mgomo yalishambuliwa kwa mawe na bajaj na bodaboda nazo zilijikuta kwenye kadhia hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva Tanzania, Abdallah Lubala, alisema madereva walichukizwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wao kwa tuhuma ambazo hazikuwa na ukweli.
Alisema juzi majira ya saa moja jioni viongozi wa madereva, akiwemo yeye mwenyewe walitakiwa kuripoti katika kituo cha polisi kilichopo ndani ya Kituo cha Mabasi Ubungo, ambako baada ya kufika walihamishiwa kituo cha Magomeni na baadaye Kituo cha Polisi Kati, ambako ndiko walikolala hadi jana asubuhi walipoachiwa.
Alisema wakiwa katika kituo cha kati waliambiwa kuwa wanafanyiwa uchunguzi kwa tuhuma za kusababisha mgomo kwa madereva, jambo ambalo walilipinga na kudai kuwa jeshi hilo ndilo lilihusika na mgogoro huo.
Lubala aliwataja viongozi wenzake aliokamatwa nao kuwa ni Bonifasi Prosper, Clement Massanja, Mourice Luhumbi, Calvin Luo na Issa Kipula na kwamba mbali na kunyang’anywa vitu walivyokuwa navyo, pia walitakiwa kutoa maelezo pamoja na kuchukuliwa alama za vidole.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...