Tuesday, February 3, 2015

WEMA AKUTANA NA TUNGULI MLANGONI KWAKE

Staa wa filamu Bongo Wema Sepetu akiwa katika pozi

IMANI za kishirikina? Mshangao wa aina yake umetokea nyumbani kwa Miss Tanzania 2006 asiyechuja, Wema Abraham Sepetu ‘Madam’ baada ya kutupiwa hirizi getini kwake, Risasi Mchanganyiko lina stori kamili.
Wananchi wakishuhudia hirizi getini kwa Miss Tanzania 2006 asiyechuja, Wema Abraham Sepetu ‘Madam’.
Tukio hilo lililokusanya watu wapenda ‘ubuyu’ lilijiri alfajiri ya Jumamosi iliyopita, nyumbani kwa mlimbwende huyo, Kijitonyama-Bwawani jijini Dar baada ya mapaparazi wetu kutonywa juu ya uwepo wa tukio hilo.
TUJIUNGE NA CHANZO
“Njooni hapa kwa Wema tumekuta mfuko mweusi wa nailoni, ndani yake una hirizi, nazi zimeandikwa maandishi ya Kiarabu huku zikiwa zimevunjwavunjwa na pia kuna picha ya Diamond ndani yake,” kilisema chanzo hicho.
MAPAPARAZI WATIA TIMU
Mapaparazi wetu ambao walikuwa kwenye mizunguko yao kikazi, walitumia usafiri wa pikipiki kwenda nyumbani hapo ambapo ndani ya dakika ‘sifuri’ walikuwa wameshafika na kukuta vitu hivyo vikiwa vimezunguka na mashuhuda.
Wananchi wakizitazama kwa karibu zaidi hirizi hizo.
KILA MTU ASEMA LAKE
Wakati mapaparazi wetu walipokuwa wakidadisi juu nani aliyetupa kifurushi hicho na sababu za kufanya hivyo, mashuhuda hao kila mmoja alieleza lake.
“Sisi hatujui aliyetupa inaonekana atakuwa alikuja usiku sana lakini inaonesha mtupaji atakuwa anataka Wema na Diamond warudiane na ndiyo maana ameambatanisha na picha ya Diamond,” alisikika shuhuda mmoja huku mwingine akidakia:
“Aliyetupa hapa atakuwa ameweka zindiko ili Diamond asirudiane tena na Wema. Atakuwa anataka Diamond aendelee na Zari.”

Katika hali ya kushangaza, mlinzi wa kampuni moja inayolinda nyumbani kwa mlimbwende huyo, aliupiga teke na kuusambaratisha mfuko uliokuwa umehifadhi vitu hivyo pamoja na hirizi.

MAPAPARAZI WAMGONGEA WEMA
Ili kutaka kujua Wema amelichukuliaje tukio hilo, mapaparazi wetu waligonga geti la Wema ambapo alitoka binti mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake na kuzungumza pasipo kufungua geti akiwa anachungulia kupitia uwazi mdogo uliopo getini hapo.
Hizi ndizo hirizi zilizokutwa getini kwa Wema zikiwa na picha ya 'Diamond'.
“He mimi sifungui, Madam (Wema) hayupo kwanza naogopa hivyo vitu si vya kawaida, mimi nakwenda zangu ndani,” alisema binti huyo na kutoweka.
APIGIWA SIMU
Mapaparazi wetu walimvutia waya Madam ambapo kilongalonga chake kiliita bila ya kupokelewa, kesho yake (Jumamosi) mapaparazi walitia timu tena nyumbani hapo na kuambiwa Madam hayupo huku simu yake ikiwa haipatikani.
WAHARIRI MZIGONI
Juzi, Jumatatu wakati gazeti hili lilipokuwa linakwenda mitamboni, wahariri wa gazeti hili walifunga safari hadi nyumbani kwa Wema na kugonga getini kwake ambapo alitoka mtu wa karibu na Wema, Petit Man. Mazungumzo yakawa hivi:
Petit: Yeah karibuni.
Staa wa filamu Bongo, Wema Sepetu.
Wahariri: Tumekuja kumuona Madam, tumemkuta?
Petit: Mna miadi naye?
Wahariri: Hatuna ila we mwambie wahariri wa Global Publishers wanakuita.
Petit: Ok subirini.
(Baada ya sekunde 30)
WEMA, PETIT WATOKA NA GARI
Wakati wahariri wakiendelea kusubiri, Wema na Petit walitoka getini wakiwa na gari aina ya Murano (lile la alilopewa Diamond) ndipo wakashusha kioo ili waweze kuzungumza nao.
Mhariri: Mambo? Vipi mzima?
Wema: Mzima niambie.

Mhariri: Dakika mbili kidogo basi tuongee.
Wema: Nina haraka lakini.
Mhariri: Hata dakika moja. Ni hivi, kuna picha tumeletewa na mapaparazi wetu zinaonesha juzi hapa nyumbani kwako kuna mfuko ulitupwa hapa ukiwa na hirizi na mazagazaga yanayosadikiwa kuwa ni ya kishirikina. 

Wema: (Kwa mshtuko) Haaaah! Hapa...kwa...ngu.
Mhariri: Hapa kwako ndiyo tena ndani yake kuna picha ya Diamond.
Wema: Kwa kweli mimi...sijui...hata sielewi kama kuna kitu kama hicho kimetokea nyumbani kwangu. MABAKI YAONEKANA
Wakati wahariri wakiendelea na mazungumzo na Wema, waliona mabaki ya vipande vya nazi pembeni ya geti hilo na kumuonesha Wema ambaye alizidi kutaharuki.
“Haaah! Kweli jamani vipande vya nazi...sawa lakini mimi imani yangu haiamini hivi vitu,” alisema Wema.
Baada ya mazungumzo hayo, wahariri walimuaga Wema huku akiwa katika hali ya sintofahamu
CHANZO: GPL

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...