Friday, February 6, 2015

WATU NA VIBONDE VYAO WIKIENDI HII VODACOM PREMIER LEAGUE


 
Beki tegemeo wa Mtibwa, Salim Mbonde, akimtoka kiungo wa Yanga, Mrisho Ngassa katika mchezo wa raundi wa kwanza, ambao Yanga walikufa kwa mabao 2-0 Jamhuri, Morogoro

Ligi kuu Tanzania Bara itakuwa ikiingia raundi ya pili kesho na keshokutwa, Jumapili, ambapo Yanga watakuwa na kibarua kigumu kuwakabiri ‘baba’ lao, Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Taifa, keshokutwa Jumapili, lakini wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, yaliyofungwa na Mussa Mugosi na Ame Ali ‘Zungu’.


Wazoea vya kunyonga... Wambieni taifa hakuna vya bure kama Jamhuri. Mashabiki 'wakisave' viingilio kwenye mechi kati ya Yanga na Mtibwa, mchezo wa raundi ya kwanza pale Jamhuri. 

Katika mchezo wa keshokutwa, Yanga itaingia uwanjani ikiwa na tafsiri ya mambo mawili; Mosi ni kutaka kuendelea kukaa kileleni mwa ligi, baada kuwashusha mabingwa Azam katitati ya wiki kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union. Pili, ni kutaka kulipa kisasi cha kufungwa, kikiwa ndicho kipigo kikubwa kwao msimu huu, achilia mbali kichapo cha bao 1-0 walichopokea kutoka kwa Wakata Miwa wa Kaitaba, Kagera Sugar.
Yanga haina rekodi nzuri mbele ya wakata miwa hao wa Turiani, Manugu hasa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro lakini ikiwa Taifa, imekuwa ikipata ushindi, ambapo msimu uliopita iliichapa mabao 2-0.
Mabingwa, Azam wao watakuwa wageni wa Polisi Moro katika Dimba la Jamhuri Moro, kesho, ambapo pande zote zimeonekana kuogopana. Meneja wa Azam, Jemedar Said Kazumari amesema kuwa wanaupa kipaumbele mchezo huo kutokana na ligi kuwa ngumu na kwamba katika ligi ya sasa, hakuna timu ndogo wala kubwa, huku kocha wa Polisi, Adolf Rishard akithibitisha kuwa wataingia uwanjani kwa ‘attention’ kubwa kwani wanakumbuka maumivu ya kichapo cha mabao 3-1 katika mzunguko wa kwanza.
Simba ambao wameonekana kurejea katika kiwango chao wao watakuwa wakipepetana na Wagosi wa Ndiba, Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Coastal wanaingia kupoza machungu ya kichapo walichokumbana nacho kutoka kwa Yanga katika mchezo wa kiporo uliopigwa katikati ya wikiendi hii.
Jambo la kuvutia ni kwamba timu hizi zinakutana zikiwa na sura mbili tofauti kabisa. Zote zinaingia zikiwa chini ya makocha wapya; James Nanga kwa upande wa Coastal na si Yusup Chippo aliyekuwa nayo raundi ya kwanza huku Goran Kopunovic akiwa na Simba badala ya Patrick Phiri aliyeiongoza kwenye mchezo wa awali uliokwisha kwa sare ya 2-2.
Lakini pia Simba itakuwa na tahadhari ya hali ya juu, kwani katika sare hiyo, Coastal walitokea nyuma na kusawazisha mabao yote.
Kiungo wa Azam, Yahya Mudathir (kulia), akikwepa daruga la mchezaji wa Polisi katika mchezo wa raundi ya kwanza msimu huu. Azam ilishinda mabao 3-1.

Wakata Miwa wa Kaitaba, Kagera Sugar watataka kulipa kisasi kwa Maafande wa Mgambo Shooting kesho, ambao katika mchezo wa kwanza waliwafunga bao 1-0, huku Abuu Mtiro akikosa penalti kwa upande wa Kagera. Hivyo mchezo wa wikiendi hii, ni kufa kupona pande zote.
Mbali na hilo, Kagera wanataka kurejesha matumani, baada ya kupoteza pointi 13 katika michezo yake mitano ya mwisho, tangu wachukue ushindi mbele ya Simba , ambao ulimtimua mzambia, Patrick Phiri. Kagera watakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage, 
Shinyanga na si Kirumba, Mwanza baada ya kupokea vitisho kutoka kwa watu waliosadikika wa Toto African, ambao wana kinyongo nao tangu mwaka 2012 kwa kile kilichosemwa kuwa Kagera 'waliwabania' na kuwashusha daraja.

Mechi nyingine Jumamosi hii zitakuwa:

JKT vs Mbeya City Chamazi- Complex

Ndanda vs Stand United- Nangwanda Sijaona

Prisons vs Ruvu Shooting- Sokoine




No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...