Thursday, July 12, 2012


Rais wa chama cha Madaktari Tanzania MAT Namala Mkopi alifikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es salaam juzi kujibu mashitaka mawili yanayomkabili kuhusiana na mgomo wa madaktari Tanzania.

Akimsomea mashtaka hayo mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Kisutu Faisal Kahamba, Mwendesha mashtaka wakili mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka alisema kosa la kwanza Dr Mkopi anashitakiwa kwa kutotii amri halali ya mahakama kuu kitengo cha kazi iliyomtaka atangaze kusitisha mgomo wa madaktari.

Wakili Kweka alisema kosa hilo ni kinyume cha kanuni ya adhabu namba 124 ambapo kosa la pili linalomkabili Dr Mkopi ni kuhamasisha mgomo wa Madaktari kinyume na kanuni na adhabu ya kifungu cha 390 na kifungu cha 35.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Dr Mkopi aliyakana yote ambapo mawakili wake wanne wanaomtetea wakiongozwa na Kikondo Maulid wameomba mteja wao apatiwe dhamana ambapo hakimu mkazi Faisal Kahamba amesema dhamana ipo wazi na kutaja masharti ya dhamana hiyo ambayo yalipingwa na mawakili wa upande wa utetezi.

Masharti ya dhamana yaliyotajwa yalikua ni wadhamini wawili waajiriwa wa serikali au taasisi zinazotambulika kisheria wakiwa na vitambulisho vyao na hati ya mali isiyopungua thamani ya shilingi laki tano ambapo mawakili wa upande wa mashitaka walitaka masharti ya kukabidhi hati ya kusafiria na kuzuiwa kusafiri nje ya Dar es salaam ndio yaingizwe kwenye masharti ya dhamana.

Hali hiyo ya mvutano wa kisheria ilimlazimu hakimu huyo jana Mahakamani kuomba muda wa dakika kumi ili apitie sheria husika na baada ya hapo mahakama iliamua kumuachia Dr Mkopi kwa masharti yaliyotajwa awali ambapo hakimu alitangaza kwamba kama kuna mtu hajaridhia dhamana hiyo anaweza kukata rufaa mahakama kuu hivyo akaiahirisha kesi hiyo mpaka mwezi wa nane tarehe 6 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...