Thursday, July 19, 2012

RAIS KIKWETE, MANJI, RAGE, TFF WAWALILIA WA MV SKAGIT

 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa salamu za rambirambi, kufuatia kuzama kwa meli ya MV Skagit jana; soma Taarifa yake.



Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
"JANA tarehe 18 Julai, 2012, majira ya alasiri kumetokea ajali ya kuzama kwa meli ya MV SKAGIT katika eneo la Chumbe, Zanzibar. Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kueleka Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290. Kati yao watu wazima 250, watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.
Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano yaani JWTZ na Polisi waanze kazi ya uokoaji mara moja.
Kazi hiyo imefanywa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na meli za makampuni binafsi. Mpaka giza lilipokuwa limeingia na hivyo kazi ya uokoaji kusitishwa mpaka kutakapokucha tarehe 19 Julai, 2012, watu 136 walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa zimepatikana. Aidha, mali zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa.
Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano alizungumza na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Alimpa pole kwa ajali iliyotokea hasa kwa vifo na majeraha waliyopata Watanzania wenzetu na watu wasiokuwa raia wa Tanzania. Alimuomba afikishe salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopotelewa na jamaa zao na kuwapa pole waliopata majeraha na maumivu maungoni mwao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano alisema kuwa huu ni msiba wetu sote na kwamba majonzi yao ni majonzi yake na ya Watanzania wote. Kwa ndugu zetu waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo na kulijenga taifa letu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti tangu taarifa ya kutokea kwa ajali mpaka sasa.
Aidha, amewapongeza maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa meli binafsi, kwa juhudi kubwa walizozifanya za uokoaji wa ndugu zetu waliopatwa na maafa haya makubwa na ya aina yake. Amewataka waendeleze juhudi hizo leo na siku zijazo.
Rais amewataka wananchi wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya uokoaji inaendelea. Kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander miezi 10 iliyopita, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali.
Kutokana na ajali hiyo na msiba huu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa ya siku tatu ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo, tarehe 19 Julai, 2012.Asanteni sana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Julai, 2012,".


Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Mehboob Manji
NAYE Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yussuf Mehoboob Manji ametoa salamu za rambirambi kufuatia tukio hilo, akisema kwamba msiba huo ni wetu sote na kwamba majonzi yao ni majonzi ya wana Yanga wote na Watanzania kwa ujumla.
Manji amesema klabu ya Yanga, inawaombea wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo mbaya kwa Mwenyezi Mungu wapate ahueni na wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku za kujiletea maendeleo na ujenzi wa taifa pia.
Aidha, Manji amewaombea wale waliopoteza uhai wao katika ajali hiyo Mungu aziweke pepa peponi roho zao na pia amewataka wafiwa wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao.



NALO Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema limepokea kwa masikitiko taarifa za ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea jana (Julai 18 mwaka huu) na kupoteza maisha ya karibu abiria 100 waliokuwemo kwenye chombo hicho.
Taarifa ya Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura Mgoyo imesema kwamba, ajali hiyo mbaya iliyotokea karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar na kusababisha vifo vya watu wengi ni msiba mkubwa, si kwa wadau wa mpira wa miguu pekee, bali kwa wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo tunatoa pole na salamu za rambirambi kwa ndugu wa marehemu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na wote walioathirika na kuguswa na msiba huo mkubwa.
Kutokana na msiba huo, mechi mbili za leo kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kati ya Atletico ya Burundi na El Salam Wau ya Sudan Kusini na ile ya Mafunzo ya Zanzibar dhidi ya Tusker ya Kenya zitachezwa huku wachezaji wa timu zote wakivaa vitambaa vyeusi.
Mbali ya vitambaa hivyo, pia kutakuwa na dakika moja ya kukaa kimya kwa ajili ya kuomboleza vifo hivyo kabla ya kuanza mechi hizo zitakazochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi ya kwanza itaanza saa 8.00 mchana wakati ya pili itachezwa kuanzia saa 10.00 jioni.





Alhaj Ismail Aden Rage




NAYE Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, kwa niaba ya uongozi, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo, wanatoa salamu za rambirambi kwa wananchi wote ambao kwa namna moja au nyingine wameguswa na tukio la ajali ya boti ya Skaget iliyotokea huko Chumbe, Zanzibar.
Rage amesema katika kipindi hiki ambacho wananchi wa Tanzania wako katika msiba mzito, Simba SC inapenda kuwapa pole wote waliokumbwa na msiba huu moja kwa moja na inawaombea kwa Mungu awape moyo wenye subra.
Katika kipindi cha maombolezo, Rage amesema shughuli zote za sherehe zimesimamishwa ndani ya klabu na bendera za klabu zitapepea nusu mlingoti katika kipindi hiki cha siku tatu za maombolezo kama kilivyotangazwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika mechi inayofuata ya Kombe la Kagame keshokutwa Jumamosi dhidi ya AS VITA ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wachezaji na viongozi wa Simba watavaa vitambaa vyeusi kama ishara ya kuomboleza msiba huu mkubwa.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...