Thursday, July 12, 2012


Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet katikati akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, Jangwani mchana wa leo, kutaja kikosi cha Kombe la Kagame. Kulia ni Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa na kushoto Mwakilishi wa Kilimanjaro Beer, wadhamini wakuu wa klabu hiyo, Oscar Shelukindo

KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amewaacha kwenye kikosi kitakachoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kuanzia Jumamosi wachezaji watatu nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na Frank Damayo kwa sababu watakuwa na majukumu ya kitaifa kwa muda mrefu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana huu, makao makuu ya klabu makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Saintfiet alisema kwamba wachezaji hao watakuwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Julai 29 dhidi ya Nigeria.


Mtakatifu Tom anasoma majina

“Kwa mujibu wa kanuni natakiwa kuwaachia wachezaji siku tano kabla ya mechi, na Jumamosi wanacheza na Rwanda, Jumatatu wanarudiana na Rwanda, baada ya hapo watakuwa kwenye maandalizi ya mechi na Nigeria, kwa hivyo sitakuwa nao hata kwenye Nusu Fainali, kwa sababu hiyo nimeamua kuwaacha,”alisema.
Saintfiet alisema amemtema pia Nahodha wa klabu hiyo, Nsajigwa Shadrack katika kikosi cha wachezaji 20, lakini amesema mchezaji huyo ni muhimu na atakuwa naye kwenye Ligi Kuu.
Amewataja wachezaji aliowateua baada ya kushauriana na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani kuwa ni; makipa Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan, Idrisa Assenga, Hamisi Kiiza na washambuliaji Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
Yanga, ambao ndio mabingwa watetezi wa Kagame, watafungua dimba na mabingwa wa Burundi, Atletico FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

KIKOSI CHA YANGA KAGAME;
Makipa; Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’
Mabeki; Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika
Viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan na Idrisa Assenga.
Washambuliaji; Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.

Mtakatifu Tom akizungumza na Waandishi hapo

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...